PBZ yachangamkia fursa ya ubadilishaji fedha za kigeni

Monday March 11 2019

By Muhammed Khamis, mwananchi [email protected]

Unguja. Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) Juma Ali amesema kuanzishwa kwa mfumo mpya wa ubadilishaji wa fedha za kigeni ni fursa mpya ya biashara kwa benki hiyo.

Ali ameyasema hayo leo Jumatatu Machi 11, 2019 mjini Unguja wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema benki hiyo imejipanga vyema na kwamba itafanya kazi hiyo ya ubadilishaji wa fedha kwa kiwango cha kisasa zaidi ili kuepusha changamoto za hapa na pale.

Mkurugenzi huyo amesema kwa vile utaratibu wa utoaji wa huduma hiyo kwao ni mpya lakini tayari wamewaandaa  wafanyakazi wao watakaohusika na huduma hiyo.

Pamoja na hayo amesema hatua ya awali wataanza na maduka mawili ambayo yatakua eneo la Darajani Unguja na Bustani ya Forodhani huku wiki moja baadaye watasambaza maduka mengine kwenye maeneo tofauti.

Ali amesema hakuna mtu atakayeruhusiwa kubadili fedha bila ya kuwa na kitambulisho ambacho kitamtambulisha yeye ni nani na atokea wapi.

Advertisement