Pamba za mamilioni zateketea kwa moto Tanzania

Muktasari:

Tangu msimu wa ununuzi wa pamba uzinduliwe Mei 2, 2019, kazi ya kununua zao hilo inasuasua kutokana na kampuni za ununuzi kusita kulipa bei elekezi ya S1, 200 iliyotangazwa na Serikali kutokana na bei ya zao hilo kushuka kwenye soko la dunia.

Simiyu. Kilo 94, 000 za pamba zenye thamani ya zaidi ya Sh112.8 milioni zilizohifadhiwa katika ghala la chama cha ushiriki cha msingi (Amcos) kijiji cha Shinyanga Mwenge nchini Tanzania zimeteketea kwa moto.

Ofisa Kilimo wilaya ya Maswa, Robert Urassa amesema ofisi yake inaendelea na tathmini kujua thamani halisi ya mali na pamba iliyoteketea na hasara iliyopatikana.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumatatu Julai 15, 2019, Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha Shinyanga Mwenge, Tungu Ngeleja amesema uchunguzi wa awali umebaini moto huo umetokana na kijiti cha kiberiti kilichorushwa na watoto waliokuwa wakicheza jirani na ghala hilo.

“Moto huo ulipenya na kuingia ndani ya ghala kutokana na eneo la chini la ghala kuwa wazi,” amesema Ngeleja

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Dk Fredrick Sagamiko ameiambia Mwananchi vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea na uchunguzi wa kina kuhusu tukio hilo lililoibua gofu miongoni mwa wakulima, Amcos na wanunuzi.

“Siwezi kusema lolote kwa sasa kwa sababu tathmini na uchunguzi wa tukio hili inaendelea; nawasihi wananchi na wakulima wawe watulivu na asitokee mtu kutumia vibaya tukio hili,” alisema Dk Sagamiko

Mmoja wa wakulima ambao pamba yao imeteketea katika janga hilo, Amos Masunga ameiomba Serikali na mamlaka zingine zinazohusika kuhakikisha wakulima waliouza pamba yao iliyoteketea kwa mkopo wanalipwa fedha zao.

“Tuliuza pamba kwa mkopo hadi ghala linateketea tulikuwa hatujalipwa fedha zetu. Tunaiomba Serikali ihakikihse tunalipwa,” amesema Masunga

Akizungumza na Mwananchi, Kamanda wa Polisi mkoa wa Simiyu, William Mkonda amesema hajapokea taarifa za tukio hilo kwa sababu yuko safarini mkoani Geita ambako kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa nyumba za makazi ya Polisi iliyoongozwa na Rais John Magufuli leo Julai 15, 2019.