Papa Wemba asisitiza upendo Afrika Mashariki

Monday November 9 2015

Mwanamuziki, Papa Wemba akitumbuiza katika

Mwanamuziki, Papa Wemba akitumbuiza katika Tamasha la Karibu Music Festival lililofanyika Bagamoyo jana. Picha na Herieth Makwetta 

By Herieth Makwetta, Mwananchi

Bagamoyo. Mwanamuziki kutoka DR Kongo mwenye makazi yake nchini Ufaransa, Papa Wemba amesema upendo ni kitendo kinachopaswa kuonyeshwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki ili kukuza maendeleo katika sekta mbalimbali za kijamii na kiuchumi.

Papa Wemba alisema hayo usiku wa kuamkia jana wakati akifanya onyesho kubwa la kihistoria katika Tamasha la Karibu Music Festival linalofanyika kwenye Viwanja vya Mwanakalenge vilivyopo Bagamoyo mkoani Pwani.

Mkali huyo wa wimbo wa “Show Me The Way” alisema japokuwa hii ni mara yake ya pili kufika nchini Tanzania, anaamini kwamba muziki unazidi kukua nchini, hivyo kwa kuungana pamoja wanamuziki wa Afrika Mashariki watafanikiwa kuvuka katika bara la Afrika.

Alisema mpaka sasa anashuhudia wanamuziki wengi kutoka Afrika Mashariki kazi zao zikionyeshwa katika vituo mbalimbali vya televisheni nchini Ufaransa ikiwemo Trace TV na vituo kadhaa vikubwa duniani jambo linaloonyesha kukua kwa muziki huo.

“Kuna wanamuziki wanafanya vizuri mfano Diamond Platnumz na Ali Kiba, hawa kazi zao zinaonekana. Kuna Sauti Soul, Jose Chameleon na sasa ni Christian Bella katika muziki wa dansi Tanzania, kwa kweli nimefurahi kufika Bagamoyo na tunashukuru kwa walioandaa hili tamasha ni zuri na jipya la kimataifa kwa hapa Tanzania,” alisema Papa Wemba kabla ya kuimba wimbo wake wa Show Me The Way.

Katika shoo yake, Papa Wemba aliimba nyimbo tano ambazo zilipokelewa vizuri na mashabiki waliohudhuria tamasha hilo kwa siku ya pili.

Akiwa jukwaani Papa Wemba aliongozana na wapiga vyombo wake, sambamba na madansa wanne wa kike ambao walionyesha makali yao kwa kunyonga viuno vyao kwa staili mpya ambayo Watanzania wengi hawakuwahi kuiona kabla. Wasanii wengine waliotumbuiza sambamba na Papa Wemba ni pamoja na John Kitime, Jikhoman Afrikabisa Band, The Arts Band, Brian Mugenyi (Jazz ),

Damian Soul ambaye aliimba nyimbo kadhaa huku mashabiki wake wakimtaka arudie na kuimba nyimbo ambazo alikuwa bado hajaziimba, kundi la Weusi lilipokea jukwaa kutoka kwa Papa Wemba saa 7:30 usiku na kukamilisha burudani ya muziki majira ya saa 9:00 usiku.

Pia lilitumbuizwa na mwanamuziki na balozi wa kutetea haki za watoto Afrika Kusini, Bo Denim ‘Bo’.

Advertisement