Papa amteua Nkwande kuwa Askofu Mkuu Mwanza

Askofu Renatus Nkwande

Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa katoliki Duniani, Papa Francis ameteua Askofu Renatus Nkwande wa Jimbo Katoliki la Bunda kuwa Askofu mkuu wa Jimbo Kuu la Mwanza.

Habari kutoka makao makuu ya kanisa hilo, Vatican zilizonukuliwa na Idhaa ya Kiswahili ya Redio Vatican, zimesema askofu Nkwande anakwenda kuziba nafasi iliyoachwa wazi, baada Papa Francis kumteua Yuda Ruwa'ichi kuwa Askofu mkuu mwandamizi katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Juni 21, mwaka jana.

Askofu Nkwande alipata upadri Julai 2,1995 na Novemba 27, 2010 akateuliwa na Papa Benedict XVI kuwa askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki la Bunda.

Aliwekwa wakfu na Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, kuwa Askofu wa Bunda Februari 20, 2011.

Askofu mkuu mteule Nkwande alizaliwa Novemba 12, 1965, katika Parokia ya Sumve, Mwanza

Alipata masomo yake ya sekondari katika Seminari ya Makoko, Musoma na baadaye Nyegezi, Mwanza. Mwaka 1987 alijiunga na Seminari Kuu ya Kibosho, Moshi, kwa ajili ya masomo ya falsafa na baadaye mwaka 1989 aliendelea na masomo ya Teolojia katika Seminari kuu ya Segerea, Dar es Salaam.

Tangu alipopadirishwa amefanya shughuli mbalimbali za kichungaji kama paroko msaidizi, Gombera wa Seminari ndogo ya Nyegezi na na mwaka 2002 hadi 2005 alikwenda Roma kwa masomo ya Sheria za Kanisa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana.

Mwaka 2008 hadi 2009 alikuwa ni makamu wa askofu, Mwanza na mwaka 2009 aliteuliwa kuwa msimamizi wa Kitume wa Jimbo kuu la Mwanza baada ya kifo cha Askofu Mkuu Anthony Mayala