Petroli ilivyoua mpangaji siku ya kwanza

Moshi. Ni simulizi inayoumiza wengi, baada ya kubainika kuwa mmoja wa watu watano waliofariki dunia kwa kulipukiwa na moto wa petroli wilayani Same, ndio kwanza alikuwa amehamia katika nyumba iliyohusika na ajali hiyo.

Mtu huyo alikuwa mpangaji ambaye hakufaidi kodi yake aliyokuwa amelipia, kwani alifariki siku hiyo hiyo akijaribu kuwaokoa majirani katika nyumba hiyo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Hamis Issah alimtaja mpangaji huyo kuwa ni Ernest Masawe ambaye aliingia katika nyumba hiyo siku ya tukio na alifariki wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC mjini Moshi.

Katika tukio hilo ambalo lilitokea Machi 7 kwenye Kijiji cha Marwa, Kata ya Ruvu, walifariki watu watano ambapo wanne ni ndugu wa familia moja.

Ndugu hao ni Christina Mndeme (40), mdogo wake Natujwa Justine (26) na watoto wake wawili ambao ni Jamila Amiri (4) na Jonson Rahim (2).

Hassan Mmari, ambaye ni ndugu wa marehemu wanne wa familia hiyo, alisema Masawe alikumbwa na mauti baada ya kuingia ndani kumsaidia mwenye nyumba wakati mlipuko ulipotokea.

“Masawe ni mpangaji ambaye aliingia kwenye nyumba siku ya tukio na alipatwa na maafa hayo baada ya kuingia ndani kumsaidia mwenye nyumba ambaye ni shemeji yangu, hali iliyosababisha na yeye kushika moto na kuungua,” alisema.

Akielezea mazingira ya tukio hilo, Mmari alisema siku ya tukio, Christina ambaye ni marehemu kwa sasa alikuwa akimpimia mteja wake mafuta ya petroli huku kukiwa na jiko pembeni.

Alisema wakati anampimia petroli ilishika moto na kumtaka mdogo wake kuuzima moto kwa kutumia maji.

“Wakati anapima mafuta, petroli ilishika moto, akamwambia mdogo wake zima huo moto wakati watoto wawili wamelala na alipojaribu kuuzima haukuzimika, ndipo alipomwambia aumwagie maji jambo ambalo lilisababisha mlipuko mkubwa na maafa hayo kutokea,” alisema Mmari.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Marwa, Elifuraha Mason alisema Masawe alifika katika kijiji hicho na kupanga nyumba ili kufanya shughuli za kilimo katika msimu huu wa masika.

Alisema maziko ya ndugu wa familia moja yatafanyika leo wilayani humo huku Masawe akitarajiwa kuzikwa kesho wilayani Rombo.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo la tukio, Kamanda Issah aliutaka uongozi wa Kata ya Ruvu kukomesha biashara holela ya mafuta majumbani.

“Muuguzi wa Zahanati ya Marwa, alikuwa akifanya biashara ya kuuza mafuta ya petroli baada ya kazi, na siku ya tukio akiwa nyumbani akipika chakula alifika kijana ambaye alihitaji mafuta hayo,” alisema Issah wakati akizungumzia namna tukio hilo lilivyotokea

“Kabla hajamaliza kumpimia petroli ilishika moto na kusababisha mlipuko, sasa niutake uongozi wa kata hii kukomesha biashara hii majumbani kwani ni hatari kwa usalama wa maisha.”