Petroli yaadimika Zanzibar

Muktasari:

Dereva wa gari la abiria lifanyalo safari zake kati ya Unguja Mjini na Bububu, Awadhi Abdallah alisema mara nyingine hulazimika kupanga foleni kwenye vituo vya mafuta kutokana na uhaba huo.

Unguja. Wananchi visiwani hapa wamelalamikia upatikanaji usioridhisha wa mafuta aina ya petroli kwa zaidi ya siku tatu sasa.

Baadhi ya wananchi walisema hali hiyo imesababisha usumbufu mkubwa, hasa kwa wanaotumia vyombo vya moto na abiria.

Mmoja wa wananchi hao, Abdallah Said alisema imekuwa jambo la kawaida kwa visiwa vya Zanzibar kuwa na uhaba wa huduma hiyo mara kwa mara, jambo ambalo linahitaji kuangaliwa kwa umakini mkubwa.

Dereva wa gari la abiria lifanyalo safari zake kati ya Unguja Mjini na Bububu, Awadhi Abdallah alisema mara nyingine hulazimika kupanga foleni kwenye vituo vya mafuta kutokana na uhaba huo.

Kwa masharti ya kutotajwa majina baadhi ya wauzaji katkavituo vya mafuta walisema hawaridhishwi na hali hiyo, lakini hawana cha kufaya hivyo wanasubiri shehena ya mafuta kutoka nje iingie.

Hata hivyo, walilisema hali imeanza kurudi kuwa ya kawaida kwa baadhi ya vituo na wana amini mpaka kesho huenda kila kitu kikawa sawa.

Akizungumzia hali hiyo, mkugenzi wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Mafuta Zanzibar (Zura), Haji Kali Haji alisema hali hiyo inatokana na kuchelewa kuingia mafuta kutoka nje kinyume cha makubaliano yao na kampuni inayohusika.

Alisema kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imeipiga faini kampuni ya United Petroleum (UP) ya dola 20,000 za Kimarekani kutokana na kuchelewesha kuingiza mafuta visiwani hapa na kusababisha usumbufu kwa wananchi.

Alisema kwa mujibu wa sheria na makubaliano na kumpuni hiyo, ikishindwa kufanya kazi ipasavyo inalazimika kulipa faini hiyo si zaidi ya wiki mbili tangu kutangazwa kwake.

Hata hivyo, alisema mafuta yameanza kuingizwa na kampuni nyingine ya Zanzibar Petroleum pamoja na Gapco na yameanza kusambazwa katika vituo vya kuuzia.