Pierre Konki Liquid kuambatana na wabunge 48 kwenda Misri

Tuesday June 18 2019

By Fidelis Butahe, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema wabunge 48 watakwenda kuishangilia timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ katika Fainali za Mataifa ya Afika (AFCON) zinazofanyika nchini Misri wakiambatana na Peter Mollel maarufu Pierre Konki Liquid.

Konki Liquid, Pierre, mama nakufa, chii ni utambulisho wa Mollel, mwanaume aliyeishika mitandao ya kijamii kutokana na vichekesho vyake.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Jumanne Juni 18, 2019 Ndugai amesema wataambatana na mchekeshaji huyo katika fainali hizo huku akiwataka wabunge zaidi kujiandikisha ili kwenda Misri.

“Hizi fainali ni muhimu na ninawashauri wabunge ambao hawajajiandikisha wafanye hivyo ili tukaishangilie timu yetu na kutembelea maeneno mbalimbali huko Misri,” amesema Ndugai.

Wiki iliyopita Ndugai alisema wabunge wanaotaka kukaa siku nne Misri wanatakiwa kulipia Dola 720 za Marekani (sawa na Sh1.7 milioni), wanaotaka kukaa siku 10 watapaswa kulipia Dola 1,490 (sawa na Sh3.5 milioni).

Katika fainali hizo zitakazoanza Juni 21 hadi Julai 19, 2019, Taifa Stars imepangwa kundi moja na Algeria, Senegal na Kenya.

Advertisement

Msafara wa wachezaji 32 wa Taifa Stars uliondoka nchini Juni 7, 2019  kwenda Cairo kuweka kambi ya maandalizi ya mwisho ya fainali hizo na tayari timu hiyo imeshacheza mechi mbili za kirafiki na Misri na Zimbabwe.


Advertisement