Pinda atangaza rasmi kuwania urais

Thursday October 23 2014Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda 

By Suzan Mwillo na Boniface Meena, Mwananchi

Dar es Salaam. Siyo tetesi tena. Sasa ni rasmi kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye amekuwa akitajwa kuwania urais amethibitisha wazi kuwa atagombea kiti hicho katika uchaguzi mkuu mwakani.

Alitoa uthibitisho huo juzi akiwa London, Uingereza ambako yuko katika shughuli za kikazi. Hatua hiyo inaondoa uvumi ambao umekuwapo kwa takriban miezi mitatu sasa kwamba naye tayari ameingia katika kinyang’anyiro hicho.

Pinda aliweka wazi nia ya kuelekea Ikulu akisisitiza kuwa hajatangaza rasmi lakini akasema kuwa ameanza harakati hizo ‘kimyakimya’. Alikuwa akijibu moja ya maswali aliyoulizwa katika Kipindi cha Dira ya Dunia kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC).

Alitamka rasmi kuwania nafasi hiyo baada ya kuulizwa kuwa anafikiri ni kiongozi gani anayefaa kurithi mikoba itakayoachwa na Rais Jakaya Kikwete.

“Mikoba ya Rais Kikwete inaweza kuchukuliwa na yeyote atakayeonekana mwisho wa safari kwa utaratibu wa chama na ndani ya Serikali .... kama anafaa. Waliojitokeza sasa ni wengi na mimi ninadhani ni vizuri,” alisema Pinda.

Alipoulizwa kama yupo miongoni mwa wengi alisema, “… umesikia kama nimo … basi tukubali hilo na yeye Waziri Mkuu yumo. Hao wote waliojitokeza pamoja na Waziri Mkuu aliyejitokeza ni katika jitihada za kusema hebu Watanzania nitazameni je, mnaona nafaa au hapana?”

Advertisement

“……..fanyeni hivyo kwa mwingine na mwingine, mwisho wa yote zile kura zitakazopatikana kwenye mkutano mkuu kama ni kutokana na chama kile kinachotawala na hatimaye Watanzania watakaojitokeza kupiga kura Oktoba kutokana na wagombea watakaojitokeza kutoka kwenye vyama mbalimbali huyo ndiye tutakayempata kama rais. Hivyo natangaza nia hiyo kimyakimya.”

Kiongozi huyo atakuwa wa pili kutangaza nia hiyo kupitia vyombo vya habari vya kimataifa, baada ya Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba.

Alitangaza nia hiyo Julai 2, 2014, alipokuwa Uingereza katika mkutano wa sekta ya mawasiliano baada ya kuhojiwa kwenye kipindi hicho hicho cha Dira ya Dunia.

Urais CCM

Kuingia kwa Pinda katika mbio za urais kupitia CCM tayari kumebadili mwelekeo wa kinyang’anyiro cha nafasi hiyo kubwa ya uongozi nchini kutokana kuzigawa baadhi ya kambi za wagombea ambao walikuwa wakitajwa kwa muda mrefu kabla yake.

Wengine ambao wamekuwa wakitajwa kuwania nafasi hiyo kupitia CCM ni Waziri Mkuu wa zamani Edward Lowassa, Waziri Mkuu Mstaafu Frederick Sumaye, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya, Mbunge wa Songea Mjini, Dk Emmanuel Nchimbi na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Steven Wassira, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja na Mbunge wa Nzega, Dk Hamis Kigwangalla.

Nguvu ya Pinda

Baadhi ya wapiga debe wa Pinda wakiongozwa na Mwenyekiti wa Mamlaka za Mitaa Tanzania (Alat), ambaye pia ni Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Dk Didas Masaburi, wamekuwa wakiweka kambi zao Dodoma kila kunapokuwa na vikao rasmi vya CCM ili kuwashawishi wajumbe wa vikao vya juu vya chama hicho wamuunge mkono.

Wakati wa vikao vya CC na NEC vya CCM vilivyomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma, kundi la wafuasi wa Pinda likiongozwa na Dk Masaburi lilikuwa mjini humo kuendelea na jitihada za kusaka wafuasi.

Harakati hizo zinaweza kuwa ndiyo maana ya kauli ya Pinda pale aliposema kwamba tayari ametangaza ‘kimyakimya’ nia yake ya kugombea nafasi hiyo.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana anaunga mkono msimamo wa Pinda na wengine waliojitangaza katika chama chake huku akivilaumu vyama vya upinzani kwa wagombea wao kukaa kimya badala ya kujitokeza ili wananchi wawapime kama wa CCM wanavyofanya.

Kuhusu Pinda, Dk Bana alisema: “Ni mzoefu amekaa Ikulu muda mrefu na kwa wadhifa wake, si vibaya kujitangaza kwani anayejitangaza wananchi wanapata muda wa kumpima na chama pia kinampima tofauti na wale ambao hawajitangazi ambao ni hatari sana kwa kuwa wanapita chinichini kutoa rushwa.”

Kuhusu upinzani, alisema: “Sijui upinzani wana matatizo gani, ningefurahi kuona (Halima) Mdee, (John) Mnyika au (Willbrod) Dk Slaa wanajitokeza ili wananchi wawapime kwani Dk Slaa wa 2010 siyo Dk Slaa wa sasa. Wakijitokeza italeta uhai kwenye hizi harakati na wananchi watakuwa na nafasi nzuri ya kuwapima,” alisema na kuongeza: “Upinzani wanapokaa kimya wanatunyima fursa wananchi kuwapima.”

Manung’uniko

Tangu kuanza kwa tetesi kwamba Pinda ameingia katika kinyang’anyiro cha urais, kumekuwa na malalamiko ya chinichini dhidi yake kwamba amekuwa akicheza rafu kama ambazo ziliwafanya na makada wenzake wenye nia sawa na yake kufungiwa na Kamati Kuu ya CCM.

Itakumbukwa kwamba makada sita wa chama hicho ambao ni Sumaye, Lowassa, Membe, Makamba, Wasira na Ngeleja wanatumikia adhabu na wapo chini ya uangalizi wa chama hicho baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kuanza kampeni za urais kabla ya muda kutangazwa.

Baadhi ya wagombea na makada wa CCM wamekuwa wakidai kuwa Pinda naye anacheza rafu hivyo kutaka ashughulikiwe, lakini wengine wamekwenda mbali zaidi na kuhoji ushiriki wake katika Kikao cha Kamati Kuu ambacho kilitoa adhabu hiyo ilhali akijua kwamba naye atakuja kugombea.

Makamba, Kigwangalla

Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba na Mbunge wa Nzega, Dk Hamisi Kikwangalla wamesema wanamkaribisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda katika mpambano wa kuwania safari ya kwenda Ikulu kupitia CCM.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, Makamba na Kigwangalla walionekana kutostushwa na uamuzi wa Pinda kuingia rasmi katika mbio hizo huku wakisema siyo tishio kwao.

Makamba kwa upande wake alisema hakuna cha ajabu kwa Pinda kuwania nafasi hiyo kwani 1995 alijitokeza Cleopa Msuya ambaye alikuwa pia waziri mkuu kupambana na mawaziri wengine kama Jakaya Kikwete na Edward Lowassa lakini alishindwa na Benjamin Mkapa ambaye alipitishwa.

Alisema pia mwaka 2005 alijitokeza Waziri Mkuu, Frederick Sumaye dhidi ya mawaziri wengine wadogo, lakini walimshinda.

“Mara zote hizo wagombea wengine walifanikiwa dhidi ya mawaziri wakuu. Nafasi za madaraka ya kiserikali hazina nafasi katika uteuzi wa wagombea ndani ya CCM,” alisema Makamba.

Makamba ambaye pia ni Mbunge wa Bumbuli alisema anamkaribisha ili wapimane ubavu lakini akasema ni muhimu kuanzia sasa hadi Mei mwakani, harakati hizo zisiathiri kazi za Serikali hasa ikizingatiwa kuwa Pinda ndiye msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali.

Dk Kigwangalla ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inayosimamia Ofisi ya Waziri Mkuu alisema haogopi mgombea hata mmoja, hata akiwa na cheo kikubwa au kidogo kwake si tishio.

“Waziri Mkuu anakaribishwa kwenye mbio hizi na asifikiri zitakuwa rahisi kwani watu tumejipanga na tuna mikakati ya kushinda,” alisema Kigwangalla.

Hata hivyo, Dk Kikwangalla alisema kuingia kwa Pinda kunaweza kuharibu mchakato mzima kwenye chama kwa kuwa ni mmoja wa watu wanaotoa uamuzi hasa ikizingatiwa kuwa kwa nafasi yake, anaingia kwenye Kamati Kuu na Halmashauri Kuu.

“Waziri Mkuu yuko kwenye nafasi ya kutuchuja, hivyo ni kama kusema refa ameamua kucheza kitu ambacho ni tatizo. Kitendo cha kutaka uongozi katika nafasi kama yake kitaondoa usawa,” alisema Dk Kikwangalla.

Advertisement