Pingamizi la Serikali kesi ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi latupwa

Thursday February 14 2019

 

By James Magai, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imetupilia mbali pingamizi la awali dhidi ya kesi ya kikatiba ya kupinga wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Atuganile Ngwala aliyesikiliza pingamizi hilo la Serikali.

Kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2018, ilifunguliwa na Bob Wangwe dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Katika kesi hiyo, Wangwe alikuwa anapinga wakurugenzi hao wa halmashauri kuwa wasimamizi wa uchaguzi kwa niaba ya NEC pamoja na mambo mengine.

Pia alidai kuwa wakurugenzi hao ni wateule wa Rais ambaye pia ni mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo, AG aliweka pingamizi la awali akiiomba mahakama hiyo iitupilie mbali kesi hiyo kwa madai kuwa kesi hizo zimefunguliwa isivyo sahihi kisheria.Katika hoja nyingine, AG alikuwa akidai kuwa hati ya kiapo kinachounga mkono kesi hiyo kina kasoro za kisheria na kwamba hazina maana bali ni za kuudhi tu zenye kupoteza muda wa mahakama bure.

Hoja hizo zilipingwa na wakili wa Wangwe, Fatma Karume, pamoja na mambo mengine akidai kuwa imefunguliwa kihalali na kwa mujibu wa sheria.

Akitoa uamuzi wake jana, Jaji Ngwala alikubaliana na hoja za mdai na akaamua kutupilia mbali hoja za pingamizi hilo la Serikali akisema kuwa hazina mashiko.

Kwa uamuzi huo, kesi hiyo sasa itapangiwa tarehe ya kusikilizwa mbele ya jopo la majaji watatu na baada ya kusikiliza hoja za pande zote ndipo itakapotoa uamuzi wake wa ama kuwaengua wakurugenzi hao kusimamia uchaguzi au la.Advertisement