Pipi zadaiwa kuwa na dawa za kulevya

Muktasari:

Kamishna Msaidizi wa DCEA, Ziliwa Machibya alisema wanaotengeneza dawa hizo lengo lao ni kukwepa mkono wa sheria.


Dar es Salaam. Mamlaka ya Kupambana na Kuzuia Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imesema watengenezaji wa dawa za kulevya sasa wamebuni mbinu mpya ya kutengeneza dawa aina ya New Cycle Active Substances (NPS) inayotajwa kuwa na athari kama za heroin, cocaine, bangi na mirungi.

Akizungumza na Mwananchi baada ya mkutano wa mamlaka hiyo wa kuandaa kongamano la wasanii la kujadili na kutoa elimu kuhusu matumizi ya dawa hiyo litakalofanyika kesho, Kamishna Msaidizi wa DCEA, Ziliwa Machibya alisema wanaotengeneza dawa hizo lengo lao ni kukwepa mkono wa sheria.

“Mfano hapa nchini kuna orodha ya dawa ya cocaine, heroin, bangi na mirungi lakini wao wanatengeneza nyingine mpya ambayo haipo katika orodha na ina madhara kama zilivyo dawa nyingine,” alisema.

Machibya, ambaye pia ni mkemia wa DCEA alisema utengenezaji wa dawa hiyo unatumia malighafi ya kemikali bashirifu ambayo hutumika viwandani lakini ikichepushwa inatengeneza dawa za kulevya.

“Mtu akiwa na kemikali bashirifu anaweza kutengeneza dawa hizi akiwa nyumbani na kuingiza sokoni na zinaweza kuwa katika mfumo wa pipi, unga na vidonge au mfumo wowote ili mtumiaji azitumie,” alisema.

Alibainisha kuwa wana taarifa za mfumuko wa dawa hizo mpya, wamejipanga kufuatilia mitaani ili kubaini kiwango kilichopo na kilichoenea.

“Dunia inapaswa kutambua kwa sasa dawa za kulevya zimeingia katika mfumo mwingine mpya na dawa hizi zinatengenezwa pia kwa mfumo ule ule wa cocaine, heroin na bangi,” alisema.

“Dawa hiyo mpya ina athari katika mfumo wa fahamu. Jinsi mfumo wa fahamu unavyoathirika ni sawa ambavyo mtu angetumia dawa nyingine,” alisema.

Alisema dawa mpya inapotengenezwa inalenga kutumiwa na binadamu wakiwemo watoto wa shule za msingi na sekondari na kwamba kadiri inavyotumiwa athari inazidi kuongezeka kwa mhusika.

Mmoja wa wafanyakazi wa asasi ya kiraia inayofanya kazi na DCEA katika suala la kutoa elimu na kukemea dawa jina lake limehifadhiwa, alisema walikwenda katika shule mbalimbali za Dar es Salaam kwa ajili ya kuwajengea uwezo wanafunzi kuhusu matumizi ya dawa za kulevya.

Alisema katika mchakato huo walikumbana na changamoto mbalimbali, ikiwemo kubaini baadhi ya watoto kutumia dawa za kulevya katika shule mbalimbali za Dar es Salaam.