Polepole amtumia Dk Slaa kuing’oa Chadema Karatu

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humfrey Polepole akizungumza na wakazi wa Karatu kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika jana kwenye Uwanja wa CCM Wilaya ya Karatu mkoani Arusha. Picha na Mussa Juma

Muktasari:

  • Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amewataka viongozi wa Chadema wilayani Karatu kujiandaa kufanya kazi nyingine kwani uongozi wao katika jimbo hilo umefikia ukomo huku akiwataka wananchi kumfuata mbunge wao wa zamani Dk Slaa ambaye amehamia CCM.

Karatu. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole, amewataka wakazi wa Wilaya ya Karatu kumfuata mbunge wao wa zamani, Dk Wilbroad Slaa akibainisha kuwa wakati wa upinzani kuongoza jimbo la Karatu umefikia mwisho.

Akizungumza katika mkutano wa halmashauri kuu ya CCM Wilaya ya Karatu uliofanyika kwenye uwanja wa CCM wilayani humo, Polepole alisema haoni sababu wakazi wa Karatu kuendelea na Chadema, akidai chama hicho kimeshindwa kuboresha maisha yao kwa miaka 25.

Hata hivyo, Dk Slaa baada ya kuachana na Chadema hakujiunga na chama chochote cha siasa zaidi ya kutangaza kuachana na siasa za vyama. Hata baada ya kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Sweden, katibu mkuu huyo wa zamani wa Chadema hajatangaza kujiunga na chama chochote.

“Mzee wenu aliondoka tangu 2015 hivi sasa anakula bata Sweden na anachapa kazi kwelikweli na ameachana na wazinguaji na wasanii wa hicho chama,” alisema Polepole.

Alisema kutokana na utendaji kazi mzuri wa Dk Slaa, ndiyo maana Rais John Magufuli amemuongezea nchi nyingine za kuzisimamia ambazo ni Denmark, Norway na Finland.

Dk Slaa alikuwa mbunge wa kwanza wa upinzani Karatu, kuanzia mwaka 1995 hadi 2010, kumuachia kijiti Israel Natse wa Chadema mwaka 2010 hadi 2015, kuanzia mwaka huo hadi sasa mbunge wa jimbo hilo ni Wilibroad Qambaro pia wa Chadema.

Polepole alisema viongozi wa Chadema katika wilaya hiyo, wajiandae kufanya kazi nyingine kwani mwisho wao ni mwaka huu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa pamoja na udiwani na ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa 2020.

“Hakuna kazi ambayo wanafanya, nimekwenda Kata ya Kansai wamekula fedha za ujenzi wa madarasa, hapa mjini Karatu soko ni chafu, hakuna maji mjini na hawajawahi kukutana na wananchi,” alisema Polepole.

“Tangu nimekuja hapa najiuliza mnawachagua kwa nini? Nimetembelea kata na vijiji kuna shida nyingi na mimi kama msimamizi wa ilani ya CCM tutatatua kero hizo.”

Katika hatua nyingine, Polepole alisema jana baada ya kutembelea na Kata ya Kansai na kukutana na shida kubwa la maji, alimtumia ujumbe wa simu, Rais John Magufuli juu ya shida ya maji. “Baada ya wananchi kunizuia kuondoka kutokana na shida kubwa ya maji, nilimuandikia ujumbe mfupi Rais John Magufuli na baada ya muda alinijibu kuwa anatoa Sh130 milioni ili kusaidia kusambaza maji katika Kata ya Kansai,” alisema.

Alisema pia amebaini kuna tatizo kubwa la maji katika mji wa Karatu na kabla ya kuondoka atakutana na viongozi wa Mamlaka ya Maji Karatu (Karuwasa) na viongozi wa Serikali kutatua kero hiyo.

Akizungumza katika mkutano huo, mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Arusha, Loota Sanare chama hicho tawala ni imara na kinataka viongozi waadilifu ambao wataendana na sera zake.