Polepole atangaza mwisho wa Chadema Karatu

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole

Muktasari:

  • Katibu wa Itikadi wa Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amewataka viongozi wa Chadema wilaya ya Karatu kujiandaa kufanya kazi nyingine kwani miaka 25 ya kuongoza jimbo hilo imefikia kikomo

Karatu. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amewataka viongozi wa Chadema wilayani Karatu kujiandaa kufanya kazi nyingine kwani miaka 25 ya kuongoza jimbo hilo imefikia kikomo.

Akizungumza leo Jumapili Februari 10, 2019 wakati akiweka jiwe la msingi la uzinduzi tawi la CCM namba moja Karatu mjini, Polepole amesema kuanzia Januari 2019 viongozi wa serikali za mitaa na vijiji na vitongoji wa Chadema watang'oka na mwaka 2020 jimbo litarudi CCM.

"Wakati wa Karatu kuongozwa na chama cha uchochoroni umekwisha, miaka 25 ya Chadema imefikia kikomo na viongozi wa Chadema muanze kutafuta kazi nyingine,” amesema.

Polepole amesema Karatu imekuwa nyuma kimaendeleo kutokana na kukumbatia chama cha upinzani kwa miaka 25 sasa.

Jimbo la Karatu tangu mwaka 1995 linaongozwa na Chadema ambapo mbunge wa kwanza alikuwa ni Dk Willbrod Slaa ambaye kwa sasa ni balozi wa Tanzania nchini Sweden.