Polisi: Hatuna taarifa ya mikutano ya CCM, Chadema mkoani Morogoro

Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa 

Muktasari:

Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema halina taarifa ya mikutano ya CCM na Chadema iliyopangwa kufanyika maeneo tofauti mkoani humo.


Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro limesema halina taarifa ya mikutano ya CCM na Chadema iliyopangwa kufanyika maeneo tofauti mkoani humo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Juni 12, 2019 Kamanda wa polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema hawajapokea maombi ya chama chochote kufanya mkutano.

“Vyama vyote vinajua utaratibu wa kisheria kwa kuandika barua ambazo zikitufikia tutazijadili kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni na tutaeleza nini kifanyike. Siwezi kuzungumzia barua ambayo haijaletwa kwangu,” amesema Mutafungwa.

CCM kinatarajia kufanya mkutano wake Juni 15, 2019 kwa ajili ya uzinduzi wa kampeni ya ‘tuwe pamoja tusikubali kugawanyika Morogoro ya Kijani Inawezekana’, huku Chadema kikipanga kufanya mkutano wake Juni 16, 2019 katika jimbo la Morogoro mjini huku mgeni rasmi akitajwa kuwa mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Wakati polisi wakieleza hayo katibu wa CCM mkoani Morogoro, Shaka Hamdu Shaka na katibu wa Chadema katika Mkoa huo, Barnabas Okola, wamesema watatoa taarifa hizo.

Shaka amesema CCM wanafanya kikao cha kawaida katika uwanja wa Jamhuri kwa madai kuwa wanachama wa chama hicho hawaonekani katika jengo la Mkoa la chama hicho tawala.

“CCM hatufanyi kampeni ya uchaguzi kwani muda bado tunachofanya ni kikao cha kawaida. Nia yetu ni kujitathmini  na kulinda umoja na mshikamano wetu," amesema Shaka.

Amesema katika kikao hicho wamewaalika wanachama wao wote, wakiwemo wamachinga, wajasiriamali na madereva bodaboda ili pia kusikiliza kero zinazowakabili.

Alipoulizwa kama wametoa taarifa za kufanya kikao hicho amesema wapo katika taratibu za kutoa taarifa polisi.

Okola amesema maandalizi ya mkutano wao yamekamilika na viongozi wanaendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi.

Kuhusu kutoa taarifa, Okola amesema hilo watalizingatia kwa kuwa hakihitajiki kibali ili kupewa ruhusa ya kufanya mkutano.