Polisi Kilimanjaro wanasa ndoo 60 za samaki wachanga

Godlizen Mfinanga wa kwanza kushoto, aliyekamatwa na ndoo 20 za samaki wachanga. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Jeshi la polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia mtu anayedaiwa kuwa kinara wa uvuvi haramu katika bwawa la nyumba ya Mungu mkoani Kilimanjaro baada ya kukamatwa na ndoo 60 za samaki wachanga.

Mwanga. Polisi mkoani Kilimanjaro limekamata ndoo 60 zenye ujazo wa lita 20 za samaki wachanga waliovuliwa kwa nyavu haramu (makokoro) katika bwawa la Nyumba ya Mungu wilayani Mwanga.

Akizungumzia kukamatwa kwa samaki hao, Kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Hamis Issah amesema wanamshikilia Godlizen Mfinanga(37) mkazi wa kwa Mromboo jijini Arusha ambaye ndio kinara wa kuvua samaki hao haramu pamoja na Mwidin Suleiman mkazi wa Kisongo.

Aidha Kamanda Issah amesema watuhumiwa hao wamekamatwa majira ya saa 3:30 usiku jana Jumatatu kata ya Kirwa tarafa ya Lembeni wilayani humo.

"Jeshi la polisi tunawashikilia watu wawili waliokuwa wakisafirisha samaki waliovuliwa kwa nyavu haramu katika bwawa la nyumba ya Mungu majira ya saa 3:30 usiku waliokuwa wakipelekwa  jijini Arusha," amesema Kamanda

Kamanda Issah amesema watuhumiwa hao watapelekwa kituo cha polisi Moshi Mjini huku taratibu nyingine za kufikishwa mahakamani zikiendelea.

Naye Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema mvuvi huyo amekua akiwasumbua kwa muda mrefu kwani alikua akiisababishia wilaya hiyo kupata hasara kwa miaka mingi.

"Wilaya ya mwanga ingetakiwa iwe juu katika ukusanyaji wa mapato yake lakini huyo tuliyemkamata leo ametusababishia hasara kubwa sana.”

“Hii wilaya ingekuwa na uwezo wa kukusanya mapato Sh10 bilioni kwa mwaka kama kungekuwa na uvuvi halali lakini sasa hivi tunakusanya Sh20 milioni kutokana na uvuvi haramu unaoendelea," amesema Mghwira.