Polisi Morogoro wawadaka 48 wakituhumiwa kwa mauaji, wizi

Kamanda wa polisii mkoa wa Morogoro Wilbroad Mutafungwa akionyesha watuhumiwa wanaohusika na wizi wa, pikipiki kwa waandishi wa habari, ambapo katika matukio hayo watuhumiwa 48 wanashikiliwa na jeshi la polisi Morogoro, katika matukio hayo pikipiki tatu zimekamatwa.

Muktasari:

Watuhumiwa 48 wa makosa mbalimbali yakiwemo ya mauaji na wizi wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Morogoro

Morogoro. Polisi mkoani Morogoro inawashikilia watu 48 ambao wanatuhumiwa kwa makosa mbalimbali ikiwemo ya mauaji na wizi wa pikipiki.

Kamanda wa polisi mkoani humo, Wilbroad Mutafungwa akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatano Juni 2, 2019 alisema matukio hayo yalitokea kati ya Mei 30 hadi Juni 10, 2019 katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Mutafungwa alisema katika kundi na watuhumiwa hao wa pikipiki wapo waporaji, wapokeaji mali za wizi, wakabaji na wapo wanao walengesha wale waendesha pikipiki.

Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na wengi wao wamekiri kuhusika na matukio yaliyoripotiwa ya wizi wa pikipiki..

“Katika mbinu nyingine waendesha pikipiki wamekuwa wakibeba abiria wasio waaminifu ambao wengine huonekana kabeba mkate au mzigo kumbe abiria hao ambao ni waalifu wanakuwa wamebeba jiwe kwa ajili ya kutumia kumdhuru mwendesha bodaboda,” alisema.

Kamanda Mutafungwa aliwataka waendesha bodaboda kuendelea kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi pindi wanapoona mwenzao anayefikia katika kijiwe cha bodaboda na hajasajiliwa waanze kumfuatilia na kuwajulisha polisi ili kuondoa tabia hiyo.

“Lakini jambo lingine linalifanya na kusababisha wizi kushamiri ni tabia ya waendesha bodaboda wengi kununua bila kusajili, hivyo wamiliki wote wa pikipiki kusajili kwa utaratibu uliopo,” alisema

Pia alisema baadhi ya watuhumiwa walitambulika ni wale walihusika pia na uporaji wa simu za watu.

Mmoja wa watuhumiwa aliyejitambulisha kwa jina la Emanuael Agatoni alisema alianza kuuza pikipiki za wizi tangu mwaka 2014 na amekuwa akifanya kazi hiyo kwa muda mrefu ambapo alikuwa akiuza pikipiki hizo mkoani Kilimanjaro.

“Hii kazi kwa sasa nimeiacha  ingawa niliifanya kwa muda mrefu,” alisema Agatoni