Polisi Morogoro yawasaka wabunge Chadema

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa

Muktasari:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema jeshi hilo linawasaka wabunge wawili wa Chadema, Peter Lijualikali (Kilombero) na Suzan Kiwanga wa Mlimba

 

Morogoro. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema jeshi hilo linawasaka wabunge wawili wa Chadema, Peter Lijualikali (Kilombero) na Suzan Kiwanga wa Mlimba.

Wabunge hao walikuwa miongoni mwa wanachama 13 wa Chadema walioachiwa huru na mahakama mkoani humo Januari  2019.

Waliachiwa huru kupitia kifungu cha Sheria namba 225 cha mwenendo wa makosa ya jinai baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka yaliyokuwa yanawakabili, ikiwa ni pamoja na kuchoma moto ofisi ya Sekondari ya kijiji cha Sofi Wilaya ya Malinyi.

Siku chache baada ya kuachiwa huru, polisi leo Jumatano Februari 20, 2019 imeeleza kuwa imewakamata wanachama saba kati ya 13.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mutafungwa amesema miongoni mwa wanachama wanaowatafuta ni wabunge wa chama hicho.

Amesema hivi sasa wamejipanga kwa kuwa na ushahidi na vielelezo vya kutosha vya kuwatia hatiani.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, Kiwanga amesema mahakama ilishindwa kuwatia hatiani kwa sababu polisi waliandaa ushahidi wa kupika na walishindwa kupeleka mashahidi wote mahakamani kama walivyokuwa wameahidi.

"Mimi nipo mbali lakini nimemtuma kiongozi mmoja wa chama kufuatilia. Polisi wamewakamata wenzangu kwa kuwavamia na kuwavizia majumbani jambo ambalo sio la kistaarabu wakati wangeweza kuwapelekea hati ya wito na wakaenda wenyewe" amesema Kiwanga.