Polisi Rukwa yawatawanya madereva bajaji kwa mabomu ya machozi

Muktasari:

Madereva  bajaji katika soko kuu la mkoa wa Rukwa wameendelesha mgomo wa kutoa huduma ya usafiri wakipinga agizo la serikali ya wilaya ya Sumbawanga mkoani humo la kuwataka kuwa na vitambulisho vya ujasiliamali ‘machinga.’ Vitambulisho hivyo hutolewa kila kimoja kwa Sh20,000

Sumbawanga. Polisi mkoani Rukwa wamefyatua mabomu ya machozi hewani kuwatawanya baadhi ya madereva wa bajaji wanaoendelea na mgomo wa kutoa huduma ya usafiri wakipinga kuuziwa vitambulisho vya ujasiriamali.

Tukio hilo limetokea leo Jumatano Juni 26, 2019 katika eneo la soko kuu ambapo madereva hao walikuwa wamekusanyika tangu asubuhi wakijadili hatma yao kufuatia agizo la Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga, Dk Halfan Haule la kuwataka lazima kununua vitambulisho hivyo.

Baada ya polisi kufika eneo walilokuwa wamekaa madereva hao walianza kufyatua mabomu ya machozi hewani hali iliyosababisha taharuki kwa wananchi wengine walikuwapo kwenye eneo hilo.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Mathias Nyange amekiri polisi kufyatua mabomu hewani ya kuwatawanya madereva hao, lakini amedai hawezi kuongea lolote kwa kuwa yupo kikaoni.

Mwenyekiti wa madereva wa Bajaji, Fred Mwanjali amesema wao wameamua kuendesha mgomo usio na kikomo kwani hawakubaliani na hoja ya serikali kutaka wanunue vitambulisho hivyo.

Amesema wao haviwahusu kwani ni madereva kama walivyo madereva wengine na vyombo vyao vya usafiri vimesajiliwa na vinalipia kodi zote kwa mujibu wa sheria.