Polisi Tanzania yamdaka daktari bingwa feki akiwa na dawa za magonjwa ya akili

Muktasari:

  • Mkazi wa Visiga mkoani Pwani, Moses Lucas Masoud (34) anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Ruvuma kwa kujifanya daktari bingwa akiwa na dawa mbalimbali ikiwamo za magonjwa ya akili.

Songea. Polisi Mkoa wa Ruvuma nchini wa Tanzania linamshikilia Moses Lucas Masoud (34) mkazi wa Visiga mkoani Pwani  kwa tuhuma ya kujifanya daktari bingwa wa kutibu  magonjwa  mbalimbali ya binadamu.

Inadaiwa daktari huyo feki alikuwa akitoa huduma za kitabibu katika Kanisa la Jesus Miracle Church (JMC) lililopo maeneo ya Msamala kwa Gasa katika Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma ambapo wananchi walimbaini kutoa taarifa kwa Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk Jair  Khanga.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Jumatano Agosti 14, 2019 Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma, Simon Maigwa alisema daktari huyo feki alikamatwa Agosti 13,2019 saa saba mchana katika maeneo ya Msamara kwa Gasa akiendelea na kutoa huduma za kitabibu kwa binadamu.

Alisema kabla ya kuanza kutoa huduma hiyo ya kitabibu aliingia kwenye kanisa hilo na kujitambulisha yeye ni daktari bingwa ana uwezo wa kutibu magonjwa mbalimbali ya binadamu na pia alijitambulisha yeye ni daktari anayetibu viongozi wakubwa wa Serikali ya Tanzania.

Kamanda Maigwa alidai daktari huyo feki  amekuwa akitoa huduma hiyo ya kitatibu kwa gharama kati ya Sh600,000 hadi Sh1.2 milioni kuligana na homa ya mteja wake, kitu ambacho kiliwashtua wananchi na kuanza kumtilia shaka kutokana na gharama ya matibabu ambayo anatoza kwa mgonjwa.

Alisema Polisi akishirikiana na Dk Khanga baada ya kupata taarifa  hiyo walikwenda kwenye kanisa hilo na kumkuta akiendelea kutoa huduma na alipohojiwa alikiri hana taaluma ya udaktari na hajahitimu mafunzo yoyote ya udaktari katika chuo chochote cha udaktari kinachotambulika na Serikali.

Naye Dk Khanga daktari huyo feki baada ya kukamatwa alikutwa na vifaa tiba kama vile kifaa cha kupimia shinikizo la damu (BP), kipimo cha sukari, kipimo cha malaria, kipimo cha kupima Virusi vya Ukimwi pamoja na dawa mbalimbali ikiwemo magonjwa ya akili kitu ambacho ni kinyume cha sheria ya nchi kwani anaweza kusababisha madhara makubwa kwa binadamu.