UTATA: Polisi kuuliza kabila la mtuhumiwa kwaibua mjadala

Dar es Salaam. Kwa miaka mingi, kila anayefikishwa Polisi kwa tuhuma mbalimbali pamoja na mambo mengi kwenye maelezo, hutakiwa kutaja kabila lake katika utambulisho jambo ambalo hivi karibuni, limezua mjadala baadhi ya wananchi wamehoji mantiki yake.

Kwa utaratibu wa jeshi hilo, wakati wa kuandika maelezo ya watuhumiwa kwenye utambulisho mambo muhimu yanayozingatiwa ni kosa, namba ya kesi, jina, umri, kabila, kazi na makazi.

Mjadala wa suala hilo umeibuka hivi karibuni baada ya askari wa Kituo cha Polisi cha Mburahati, Dar es Salaam kusambaza picha za wanawake zilibainisha pamoja na mambo mengine, makosa yao na makabila jambo lililolalamikiwa na wanaharakati watetezi wa haki za binadamu.

Alipoulizwa kuhusu madala huo, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro alisema suala hilo linaongozwa na Sheria ya Ushahidi.

“Wewe uliza sheria ya ushahidi inasemaje, nenda kasome hiyo sheria halafu uniulize,” alisema Sirro. Hata hivyo, mwandishi wetu hakuona kipengele kinachoelekeza watuhumiwa kutaja makabila yao.

Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kifungu cha 11(1) kinachozungumzia ukamataji inasema, “Katika ukamataji ofisa wa polisi au mtu mwingine atakayekamata atashika mwili wa mtu aliyekamatwa vinginevyo apelekwe kwenye kizuizi kwa maneno au kitendo.”

Kifungu cha 53 cha sheria hiyo kinasema, “Mtu aliye chini ya ulinzi, ofisa wa polisi hatamuuliza swali lolote au kumwambia afanye lolote kwa jambo linalohusu uchunguzi wa kosa lake, isipokuwa tu, amtajie jina na cheo chake na mtu huyo aliyejulishwa na ofisa wa Polisi kwa lugha anayoielewa kwa ufasaha katika kuandika na kuitumia.”

Mbali na sheria hiyo, Sheria ya Jeshi la Polisi, kifungu cha 32(1) inaeleza utaratibu wa kukamata na kuthibitisha uhalali wa kumkamata mtu.

Inasema, “Pale ambapo ofisa polisi anatuhumu kwamba mtu anaweza kuwa ametenda kosa kubwa, au anaamini kwamba habari imepokewa na polisi ambayo inaweza kuhusisha mtu katika kutendeka kwa kosa kubwa, lakini tuhuma hizo au imani sio kama ilivyokuwa chini ya kifungu cha 13 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, kudhibitisha uhalali wa kumkamata mtu bila hati, afisa polisi hatamuuliza maswali, isipokuwa amemfahamisha kwanza kwamba anaweza kukataa kujibu swali lolote analoulizwa na afisa polisi.”

Ofisa mmoja wa Polisi aliyezungumza na Mwananchi kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini, alisema japo hakuna kifungu cha sheria kinacholazimisha mtu kutaja kabila lake, lakini huwataka wafanye hivyo ili kujua utamaduni wake wakati wa kumdhibiti ili wasije kumvunjia heshima na haki zake kulingana na kabila na dini yake.

Baadhi ya wanasheria akiwamo wakili maarufu nchini, Fatma Karume walisema hatua hiyo haina maana yoyote, bali ni ubaguzi ulioachwa na wakoloni.

Alihoji, “ikiwa Watanzania karibu wote wanazungumza lugha ya Kiswahili, kuna haja gani tena ya kujua kabila la mtuhumiwa? Nimewahi kuitwa kutoa ushahidi, wakaniuliza kabila, nikawaambia sina kabila. Mimi ni Mzanzibari napata wapi kabila? Wanakulazimisha hata ujitambulishe kama Mswahili.”

Wakili mwingine aliyeomba asitajwe jina lake gazetini alisema, mbali na maelezo ya polisi, hata hati za mashtaka huwa na kipengele cha kikabila.

“Inatokana na kurithi sheria za kikoloni, lakini haina maana yoyote kisheria. Suala ni kufanya tu mabadiliko ya sheria. Hata mahakimu wanapochukua maelezo ya udhamini, wanakwenda mbali hadi kuuliza kabila la mtu.

“Kwenye umri wa mtu ina maana yake kuna umri kama chini ya miaka 18 au juu yake, makazi ili wajue watakupataje, lakini kabila ndiyo haieleweki ni la nini. Tatizo haijawahi kutokea mtu akahoji kitu hicho,” alisema.

Mkurugenzi wa Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Tike Mwambipile alisema mbali na kutaja makabila, alirejea tukio la Polisi wa Mburahati na kusema wanafanya makosa ya kusambaza picha za watuhumiwa na utambulisho wao kabla hata hawajafikishwa mahakamani.