Polisi wajichanganya kifo cha mwanaharakati Kenya

Thursday February 14 2019

 

Nairobi,Kenya.Wazazi na wanaharakati wamepinga taarifa ya polisi kuhusu kifo cha Mwanaharakati mashuhuri wa haki za binadamu nchini Kenya Caroline Mwatha.

Taarifa ya polisi inasema kwamba  Mwatha alikufa akiwa anatoa mimba ya miezi mitano  hospitalini.

Hata hivyo Baba yake pamoja na wanaharakati wengine wa kutetea haki za binadamu wanasema kuwa  Mwatha aliuawa kutokana na msimamo wake mkali dhidi ya mazoea ya polisi kuwaua vijana bila kujali katika mitaa ya mabanda.

Taarifa ya Idara ya upelelezi wa jinai nchini Kenya imesema Mwatha alifariki dunia wakati wa jaribio la kutoa mimba aliyokuwa nayo ya miezi mitano, na kwamba watu sita wamekamatwa.

Taarifa hiyo hata hivyo haijaeleza ni kwa nini watu hao walikamatwa, lakini ikasema kikundi hicho ni pamoja na  mmiliki wa kliniki iliyohusika.

Msemaji wa polisi Charles Owino amethibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao sita ambao miongoni mwao ni dereva taksi aliyempeleka hispitalini hapo.

Aidha polisi wanasema kuwa maiti ya Mwatha ilihifadhiwa hospitalini Februari  saba, siku ambayo marehemu anasemekana kutoweka. Kauli inayotiliwa shaka na wanaharakati wengine wa haki za binadamu.

Taarifa ya polisi inasema kuwa mwili wa marehemu uliandikishwa kwa jina tofauti na kwamba wana ushahidi wa ujumbe mfupi kati yake na daktari aliyehusika kutoa mimba yake.

Kuhusu hilo baba wa mawanaharakati huyo amesema "Amepotea kwa sababu ya kufuata ukweli, sio ugonjwa ni ukweli. Alikuwa akitetea vijana, vijana wakishikwa na polisi, Caro ndiye alikuwa akishinda polisi, anashinda polisi akiwatetea vijana waache kuuliwa.”

Vyombo vya habari nchini humo vinasema alitoweka Februari 6 na polisi imesema ilianzisha uchunguzi siku mbili baadaye, na kugundua kuwa alikuwa na mawasiliano kuhusiana na mpango wa kutoa mimba aliyokuwa nayo.

Mwatha alikuwa Ofisa Mkuu  wa Kituo cha Kijamii kinachopigania haki za binadamu cha Dandora. Kabla ya mauti yake, alikuwa akichunguza mauaji ya kiholela yaliyotekelezwa na polisi dhidi ya wakazi sita wa Dandora Oktoba mwaka uliopita.

 


Advertisement