Polisi wataka hoteli ionyeshe kamera iliyomnasa aliyejirusha ghorofani Mwanza

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro

Muktasari:

Juzi, msimamizi wa idara ya ulinzi wa jengo hilo, Bernad Kakongo alisema walikabidhi kamera za CCTV polisi zikimwonyesha mtu huyo akijirusha kutoka ghorofa ya nne.

Mwanza. Tukio la mtu kudaiwa kujirusha kutoka ghorofa ya nne katika Hoteli ya Gold Crest limeendelea kuchukua taswira mpya baada ya jeshi la polisi kutaka hoteli hiyo ionyeshe kamera iliyomnasa wakati anaingia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro jana alisisitiza kuwa mtu huyo hajajirusha na kwamba wanaendelea kuchunguza kifo chake kwani hawaamini kama alijirusha kama viongozi wa hoteli hiyo ya kifahari wanavyodai.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Kamanda Muliro alisema bado wanaendelea kufanya uchunguzi kubaini chanzo cha kifo cha mtu huyo .

“Kitendo cha wahusika wa hoteli hiyo kudai alijirusha kutoka ghorofa ya nne hatukubaliani nacho badala yake tunaendelea kufanya uchunguzi kubaini chanzo cha kifo hicho,” alisema Kamanda Muliro.

Alipoulizwa kuhusu kamera za CCTV kumwonyesha mtu huyo akiwa amejirusha, alisema polisi pia wanataka kuona kamera hizo zikimwonyesha wakati anaingia ndani ya hoteli hiyo.

“Hapo ndipo tutaamini kuwa mtu huyo amejirusha, lakini si kutuambia amejirusha wakati hawajatuonyesha alipokuwa anaingia na ukizingatia ile ni hoteli kubwa na ina ulinzi wa kutosha, kila eneo kuna kamera. Haiwezekani zisimwonyeshe wakati anaingia isipokuwa wakati anajirusha tu,” alisema.

Aliwataka wananchi wawe na subira wakati uchunguzi unaendelea na kwamba bado hawajapata ndugu wa mtu huyo.

Juzi, msimamizi wa idara ya ulinzi wa jengo hilo, Bernad Kakongo alisema walikabidhi kamera za CCTV polisi zikimwonyesha mtu huyo akijirusha kutoka ghorofa ya nne.

Alisema hawajui alipitia njia gani kwa sababu zipo njia nyingi za kuingilia zikiwemo za kukaguliwa na kuandikisha majina, lakini pia zipo za magari na wafanyakazi ambazo hazikuwa zimefungwa kamera.

Alisema kwa sasa wameimarisha ulinzi ikiwemo kufunga kamera kila eneo lakini pia wamepitisha mikakati ikiwemo ya mtu kutosimama ovyo eneo hilo na yeyote anayeingia humo iwe anakwenda kikazi, kwenye sherehe ama shughuli yeyote ni lazima ajiandikishe.

Kakongo alisema mpaka juzi hakuna ndugu aliyefika hapo kumuulizia mtu huyo ambaye hata hivyo bado hajafahamika.