Polisi yamwachia mwandishi wa Mwananchi

Muktasari:

Waandishi Jonathan Mussa wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) na Sylvanus Bulungela wa Star Tv waliokuwa wakishikiliwa na polisi wameachiwa kwa dhamana ingawa polisi wamebaki na kamera ya mwandishi wa Star Tv na simu ya Jonathan ambazo walitumia kurekodi tukio hilo

Mwanza. Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL) mkoani Mwanza, Jonathan Musa aliyekuwa akishikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusiana na taarifa za watu kudaiwa kukamatwa wakiwa na vichwa vya binadamu ameachiwa kwa dhamana.

Pamoja na Jonathan, Mwandishi Sylvanus Bulungela wa Star Tv ambaye pia alikuwa akishikiliwa naye ameachiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Alhamisi Februari 21, 2019, Kamanda Jumanne Muliro amesema Jonathan na Bulungela walishikiliwa baada ya kudaiwa kuwa chanzo cha taarifa hizo kuenea mtaani.

"Kutokana na uhalisia wa tukio na taharuki iliyokuwepo, niliagiza wote wanaowezekana kuwa chanzo cha taarifa hizo kukamatwa na kuhojiwa kupata ukweli," amesema Kamanda Muliro.

"Lakini suala lenyewe linadhaminika na nimemwagiza RCO (Mkuu wa upelelezi Mkoa) ashughulikie waachiwe kwa dhamana," ameongeza.

Taarifa hizo zilizozagaa na kuzua taharuki zilisababisha umati wa watu kujaa eneo la Kituo cha Polisi Nyakato jijini Mwanza kutaka kushuhudia vichwa hivyo na watuhumiwa.

Wakati kamanda Muliro akisema waandishi hao walishikiliwa kwa tuhuma za kuwa chanzo cha taarifa zilizoibua taharuki, mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa (RCO) wa Mwanza, Faustine Mafwere, alisema Jonathan anashikiliwa kwa kosa la kumpiga picha alipokuwa akizungumza na wananchi waliojazana nje ya kituo cha polisi Nyakato akiwataka waondoke kwa sababu hakuna mtu aliyekutwa na vichwa vya watu.

Katika maelezo yake hayo, RCO aliahidi kumwachia huru Jonathan baada ya kuandikisha maelezo.