Polisi yasema haijui Mdude Chadema alipo, mashuhuda wasimulia alivyotekwa

Muktasari:

  • Mmoja wa mashuhudia, Yahaya Said alisema Mdude akiwa ofisini kwake eneo la Vwawa, Mbozi yalifika magari mawili, aina ya Nissan yenye rangi nyeupe ambayo hayakuwa na namba za usajili.

Mbozi. Wakati Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe likisema halimshikilii mwanachama wa Chadema, Mdude Nyagali maarufu Mdude Chadema, mmoja wa majirani zake amesimulia jinsi kada huyo wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini alivyotekwa.

Mkufunzi huyo wa Chadema ni msingi, Kanda ya Kanda ya Nyasa anadaiwa kutekwa na watu wasiojulikana juzi saa 12 jioni huku taarifa za kutekwa kwake zikisambaa mitandaoni na Chadema kutoa tamko la kupotea kwake.

Mmoja wa mashuhudia, Yahaya Said alisema Mdude akiwa ofisini kwake eneo la Vwawa, Mbozi yalifika magari mawili, aina ya Nissan yenye rangi nyeupe ambayo hayakuwa na namba za usajili.

Alisema watu wanne waliteremka na, “Walimkuta kijana mmoja nje ya ofisi ya Mdude, walimkamata na kumwingiza katika mojawapo ya magari hayo na kisha kuingia ofisini na kusikika purukushani na kelele za kuomba msaada.

“Kelele hizo zilikuwa za Mdude akiomba msaada na zilifanya watu wakusanyike lakini watu hao walitoka na Mdude na kumuingiza nyuma ya moja ya magari hayo na kisha kumuachia yule kijana waliyemkuta pale nje na kuondoka na Mdude,” alisema shuhuda huyo.

Mbunge wa Mbozi (Chadema), Pascal Haonga alisema naye hatujui kada huyo amepelekwa wapi.

“Nimezungumza na RPC (Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe) amenieleza kuwa hawajui alipo na si wao waliomkamata. Tumeshatoa taarifa kwa viongozi wa Chadema nao wanaendelea kufuatilia.”

Kamanda huyo, George Kyando alipoulizwa na mwandishi wetu alisema hadi jana mchana walikuwa hawajapata taarifa zozote za tukio hilo.

“Hakuna kesi yoyote iliyoripotiwa ambayo ingehitaji kumkamata,” alisema Kyando akiwataka wahusika kutoa taarifa polisi ili jalada lifunguliwe na uchunguzi uanze.