Pongezi ya Nape kwa Waziri Makamba yaibua mjadala

Muktasari:

Marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini Tanzania ilianza kutekelezwa Juni 1, 2019 ambapo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba aliendesha utekelezaji wa marufuku hiyo iliyotolewa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Dar es Salaam. Pongezi ambazo amezitoa Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) January Makamba jinsi alivyoendesha kampeni ya marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki imeibua mjadala.

Katika ukurasa wake wa Twitter leo asubuhi Jumatatu Juni 3, 2019 Nape ameandika ujumbe akisema kazi iliyofanywa na Makamba ni mfano wa kiongozi na siyo mtawala hali iliyowafanya wachangiaji kutoa maoni tofautitofauti kuhusu ujumbe huo.

Akiwa ameambatanisha picha yake (Nape) na Makamba wakiwa wamevalia masharti ya rangi ya kijana inayotumiwa na CCM, Nape amendika, “Namna wewe na wenzako mlivyosimamia swala la mifuko ya plastiki ni mfano tosha wa utofauti kati ya kuongoza na kutawala.. Hongera sana!.”

Waziri Makamba ameongoza kampeni hiyo ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilotoa bungeni miezi kadhaa iliyopita akisema kuanzia Juni mosi, 2019, itakuwa ni marufuku kutengeneza, kuingiza, kuuza na kutumia mifuko ya plastiki kwa ajili ya kubebea bidhaa za aina yoyote na matumizi yake yatakoma Mei 31, 2019.

Baadhi ya wafuasi waliotoa maoni yao wamemtaka Nape aonyeshe na picha ya mtawala anayemzungumzia ili wajifunze zaidi katika somo lake huku Alex akimtahadharisha kuendelea ‘kutibua bahari.’

Hata hivyo, licha ya wengi kuonyesha kukubaliana na kauli yake, baadhi wametaka viongozi wa serikali za mitaa watambuliwe katika kufanikisha kampeni hiyo. 

Benard bathromeo amechangia akisema, “@JMakamba heshima yako kaka au ni kwa sababu ya mwezi mtukufu? ila hapana ni weledi tu na hekima kumbe bila kutishiwatishiwa na kuporwa kwa nguvu mambo yanawezekana aisee.”

Denis Masebu yeye amesema, alafu hata hawajatumia minguvu na wameeleweka, hiyo kazi wangepewa kina mwafulani mbona tungejificha chooni.

Kwa upande wake, Mshemo God amesema, “Nadhani ni fundisho hata kwa waliondoa bunge live na waasisi wa bao la mkono! Shame!!”

Zakayo Mepuyinywe amesema, “Mshemo utamwonea bure mh Nape kwa kuondoa bunge live, jambo lile lilikuwa juu ya uwezo wake, kwa hiyo niwasihi Watanzania wenzangu tusiendelee kumhukumu Nnauye kwa kuondoa bunge live, inatosha sasa tuzungumze mengine, kuhusu bao la mkono hii kauli nafurahi kila ninapoisikia maana.”

Muswazi Ndono amesema Nape leo hakika imekuwa muungwana,hongera nawe kwa kuwa mkweli na muwazi, bao la mkono halijafutika bado.

Naye SeaN amehoji akisema, “Kama umetuonyesha kiongozi kwanini usingetupa  na mfano wa mtawala ili tujifunze vizuri ili somo.”

JAIZA93 real chadema ameandika, “Mh. @Nnauye_Nape nimesikia kuna wabunge wenye nongwa ndani ya chama chako hawatarudi 2020, vp unalichukuliaje hili.”

Naye Shedrack Richard amesema, “Ndiyo maana ya uongozi huo kushirikisha watu badala ya kutumia ubabe na magari ya washawasha na SMG ongera January Makamba.” Huku mans akihoji kwa kusema, “Kwa hiyo unatuambia kuna tofauti ndani ya Serikali hii.”

Kwa upande wake, Othman Abdallah amesema, “Mungu ibariki Tanzania, mungu bariki chama Cha mpinduzi, mungu mbariki makamba na mzidishie ufanisi katika utekelezaji wa maendeleo nchini kwetu.”