Profesa Kabudi awatangazia fursa wenye hoteli Dar

Saturday June 15 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amewataka wamiliki na wafanyabiashara wa hoteli jijini Dar es salaam kutumia fursa ya kibiashara itakayotokana na ujio wa wageni zaidi  ya 1,000 watakaoshiriki katika mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Agosti  2019.

Profesa Kabudi ameyasema hayo leo Jumamosi Juni 15, 2019 jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na wamiliki na wafanyabiashara wa hoteli.

Amesema wizara yake itafanya kazi kwa ukaribu na wadau hao na kuwataka kutoa huduma bora.

Waziri huyo amewataka wamiliki na wafanyabiashara hao wa hoteli kuzingatia mwongozo wa Serikali uliotolewa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kuhusiana na suala la ubadilishaji wa fedha za kigeni kwa kuwataka kuwaelekeza wageni kubadilishia fedha zao benki na pia katika hoteli ambazo zimeidhinishwa kubadilisha fedha za kigeni.

“Ninyi ni watu muhimu sana katika ugeni huu wa SADC, tushirikiane kuufanya mkutano huu kuwa wa mafanikio makubwa kwa ukarimu na uzalendo wetu na hivyo kutufanya pia kuingiza kipato katika biashara zetu.”

“Tukifanya vizuri kila watakapokuwa wanakuja Tanzania kwa mikutano mingine ya mawaziri watafikia katika hoteli zetu kutokana na ukweli kuwa tutakuwa na mfululizo wa mikutano ya SADC kuanzia Agosti 2019 hadi Agosti 2020 Tanzania itakapokoma kuwa Mwenyekiti wa Mkutano huo,” amesema Profesa Kabudi

Advertisement

Ameongeza ataendelea kukutana na wadau mbalimbali pamoja na wafanyabiashara wa sekta binafsi ili kuhakikisha fursa ya kufanyika kwa mkutano wa SADC hapa nchini inawanufaisha pia wadau mbalimbali wakiwemo wajasiriamali na wafanyabiashara.

Profesa Kabudi  amesema kutokana na mkutano huo wa SADC serikali inatarajia kuingiza zaidi ya shilingi bilioni kumi pamoja na kutengeneza ajira zaidi ya elfu tano na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa hiyo.

Advertisement