Profesa Kabudi azungumzia msimamo wa EAC kuhusu ufadhili, mikopo ya China

Muktasari:

Jumuiya ya Afrika Mashariki imeiomba nchi ya China kuhakikisha kuwa ufadhili na mikopo inayotoa inalenga katika miradi ya kikanda itakayoziunganisha na kuzinufaisha nchi hizo kiuchumi.

 

-Uhusiano kati ya China na Tanzania ulianza rasmi mwaka 1964 baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kabla ya muungano, China ilikuwa na uhusiano na Tanganyika ambao ulianza siku ya Uhuru, Disemba 9, 1961.


-Uhusiano huo uliasisi na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na Rais wa China (mwenyekiti), Mao Ze Dong. Viongozi hao waliimarisha diplomasia baina ya nchi zao na kushirikiana katika maeneo mbalimbali ya kiuchumi.

Dar es Salaam. Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeiomba nchi ya China kuhakikisha ufadhili au mikopo inayotoa inalenga katika miradi ya kikanda itakayoziunganisha na kuzinufaisha nchi hizo kiuchumi.

                                                                                                 

Kauli huyo ametolewa leo Jumanne Juni 25, 2019 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Palamagamba Kabudi katika mkutano wa waratibu wa jukwaa la ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) Beijng, China.

Taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa inaeleza katika mkutano huo Profesa Palamaganda ameitaka China kuhakikisha miradi ya maendeleo inayowekeza nchini Tanzania  inakuwa na  manufaa kwa pande zote mbili.

Amesema endapo China itazisaidia kwa ufadhili au kwa mikopo nafuu kuwekeza katika miradi hasa ya miundombinu itakayoziunganisha nchi za Kiafrika kwa kiasi kikubwa itazisaidia nchi hizo kufanya biashara na kupiga hatua za kimaendeleo na kiuchumi na hivyo kujitegemea.

“Mkutano huu umekuwa na manufaa kwa kuwa nchi zenyewe za Kiafrika zimepata fursa ya kutaja baadhi ya miradi ya kipaumbele kutokana na uhitaji wa nchi husika  ambayo ni pamoja na uzalishaji wa umeme kwa kutumia maji,” amesema Profesa Kabudi

Katika mkutano huo wa siku mbili uliozikutanisha nchi  53 za Kiafrika na China zimeitaka China pia kuhakikisha kufadhili katika kuinua uwezo wa kitaaluma utakaowawezesha vijana kwa Kiafrika kujiajiri na kupata wataalam wabobezi katika masuala mbalimbali.

Waziri wa Mambo ya Nje wa China  Wang Yi amesema China haitatoa misaada yenye masharti magumu kwa nchi za Afrika, badala yake itaendeleza ushirikiano wake na Afrika katika kutekeleza miradi ya maendeleo yenye manufaa kwa pande zote mbili.

Katika hotuba hiyo, Serikali ya China imeahidi kuongeza umoja na ushirikiano kati yake na Afrika katika masuala ya kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na kudumisha amani na usalama  ili kuleta maendeleo endelevu kwa watu na kuifanya dunia kuwa mahali salama pa kuishi.

Hatua hizo ni pamoja na programu ya kuendeleza viwanda kupitia ujenzi wa maeneo maalum ya viwanda, ujenzi wa miundombinu ikiwemo nishati, reli, barabara na bandari, sambamba na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vitakavyosaidia kuzalisha nguvu kazi ya viwandani.