VIDEO: Profesa Lipumba: Mkutano mkuu ulikwishamfukuza Maalim Seif

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba amesema Maalim Seif si mwanachama wa chama hicho kwa kuwa mkutano mkuu uliazimia afukuzwe uanachama.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amefichua siri kuwa Mkutano Mkuu uliofanyika kati ya Machi 13 hadi 15 ulishaazimia kumfukuza uanachama aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Profesa Lipumba amefichua siri hiyo leo, Jumatatu Machi 18, 2019 wakati akizungumza na Mwananchi ikiwa ni muda mchache baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutoa hukumu ya kukubaliana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kumtambua mwenyekiti huyo.

Mwenyekiti huyo amesema kwa kauli moja wajumbe wa mkutano mkuu zaidi ya 700 waliazimia Maalim Seif afukuzwe uanachama kutokana na mwenendo wake dhidi ya chama hicho kikuu cha upinzani Zanzibar.

“Kilichokuwa kimebaki ni Baraza Kuu la Uongozi Taifa, kutangaza kwa umma maazimio ya mkutano mkuu uliofanyika wiki iliyopita katika Hoteli ya Lekam Buguruni. Ukweli ni kwamba Maalim Seif tulishamfukuza uanachama,” amesema Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi.