Profesa Lipumba adai CUF inapigwa vita na vyama vingine

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba 

Muktasari:

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema licha ya chama hicho kupigwa vita na vyama vingine vya siasa, hakitarudi nyuma


Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amesema licha ya chama hicho kupigwa vita na vyama vingine vya siasa, hakitarudi nyuma.

Profesa Lipumba ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Juni 8, 2019 katika mkutano wa viongozi wa chama hicho Mkoa wa Dar es Salaam kujiandaa na uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba, 2019.

Msomi huyo amesema kuelekea uchaguzi huo wamejipanga kujibu kero za wananchi na kuzishughulikia.

Amesema CUF kina kazi ya ziada kujiimarisha kutokana na  mikakati inayofanywa na vyama vingine kukipoteza.

“Chama hiki kinapigwa vita na vyama vingine (anavitaja) ambavyo vinajikita katika maeneo yetu kuwashawishi wabunge na viongozi wengine wajiunge na vyama vyao,” amesema Lipumba.

Mwenyekiti huyo amewataka viongozi watakaopewa dhamana ya kugombea katika uchaguzi huo kujipanga kuboresha maisha ya wananchi.

“Tujipange kujibu kero za wananchi, bodaboda na mama ntilie kwa kuwa ukiangalia mazingira ya biashara hayaridhishi. Chama chetu  kinatakiwa kuwa mstari wa mbele kuwaletea wananchi furaha, na haki,”amesema.

Naye naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Magdalena Sakaya amewataka viongozi hao kuachana na makundi kwa maelezo kuwa hayajengi na kupoteza matumaini ya kushinda katika chaguzi.

“Mkikaa kwenye vikao vyenu hakikisheni hakuna makundi. Chama hakiwezi kujengwa kwa makundi tunahitaji kuwa wamoja. Haya makundi yapo kwa sababu haiwezekani bendera zetu zinashushwa watu wanaangalia tu, hii inaonyesha kuna hujuma inafanywa na wanachama wenyewe.”

“CUF ndio chama pekee chenye kuleta haki, hata mkiangalia hivi sasa wakati tunapambana kuboresha maisha ya wananchi, vyama vingine vipo kwenye mgogoro na sisi ili kukiua chama chetu,” amesema Sakaya.