Profesa Lipumba ajibu mapigo ya Maalim Seif, ateua wajumbe wa bodi

Muktasari:

  • Ukitaka kutumia lugha nyepesi utasema filamu imeanza upya CUF. Ni baada ya mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kuteua wajumbe wa bodi wa wadhamini ya chama hicho

Dar es Salaam. Ukitaka kutumia lugha nyepesi utasema filamu imeanza upya CUF. Ni baada ya mwenyekiti wa chama hicho anayetambuliwa na ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba kuteua wajumbe wa bodi wa wadhamini ya chama hicho.

Ametangaza uamuzi huo leo Alhamisi Februari 21, 2019 ikiwa zimepita siku mbili tangu upande wa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad nao kuteua wajumbe hao.

Profesa Lipumba ametangaza wajumbe hao leo  katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Amewataja wajumbe hao kuwa ni Peter Malebo, Abdul Magomba, Hajra Silia, Amina Mshamu nq Aziza Daghesh , Salh Hilal Mohammed, Asha Said Suleiman, Suleiman Makame Issa na Mussa Haji Kombo.

" Wajumbe hao wameteuliwa baada ya baraza kuu la uongozi wa CUF kukutana Februari 19, 2019. Kikao hiki kilihudhuriwa na msajili msaidizi wa vyama vya siasa, Sisty Nyahoza kama taratibu zinavyotaka,” amesema Profesa Lipumba.

"Baada ya kuteua wajumbe hawa tumewasilisha barua ya maombi ya kuisajili bodi katika ofisi ya Rita (Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi) na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.”

Amefafanua kuwa wajumbe wa  bodi ya wadhamini walioteuliwa na upande wa Maalim Seif hawatambuliki kwa kuwa upande huo hauna baraza kuu la uongozi wala kamati ya utendaji.

"Kilichonisikitisha ni namna alivyowateua wajumbe hawa, yaani Maalim Seif katika huo mkutano wa uteuzi wa wajumbe alimualika Jacob (Boniface - meya wa Ubungo) na Mbatia (James-mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi) kushuhudia tukio hilo. Hivi hawa wanawajua vizuri wajumbe wa baraza kuu la CUF?

Ameongeza, “Huyu ( Maalim Seif) sio mzuri anataka kukiua chama hiki  na hana nia ya dhati dhidi ya CUF. Nawaambia bodi halali ni iliyotangazwa leo na si vinginevyo na nina imani Rita itatenda haki.”