Profesa Lipumba amtangaza mrithi wa Maalim Seif CUF

Muktasari:

  • Baraza Kuu la Uongozi wa Chama cha Wananchi (CUF), upande wa Profesa Ibrahim Lipumba limemchagua Khalifa Suleiman Khalifa kuwa katibu mkuu wa chama hicho.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amemtangaza Khalifa Suleiman Khalifa kuwa katibu mkuu wa chama hicho.

Mbali na Khalifa, Profesa Lipumba pia amemtangaza mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya kuwa naibu katibu mkuu Bara na Fakhi Suleiman Khatibu kuwa naibu katibu mkuu Zanzibar.

Profesa Lipumba amemtangaza Khalifa ambaye ni mbunge wa zamani wa Gando kuchukua nafasi ya Maalim Seif Sharif Hamad leo Jumamosi Machi 16, 2019 makao makuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam.

Katibu mkuu huyo mpya, amepatikana baada ya kuchaguliwa na Baraza Kuu la Uongozi lililokutana jana Ijumaa.

Hata hivyo, hatima ya viongozi hao wapya wa CUF akiwamo Profesa Lipumba aliyechaguliwa na mkutano mkuu Jumatano iliyopita Machi 14, 2019, itajulikana baada ya hukumu itakayotolewa Jumatatu ya Machi 18, 2019 na Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam.

Hukumu hiyo ni ya kesi iliyofunguliwa na baadhi ya wanachana wa chama hicho upande wa Maalim Seif wakipinga uhalali wa Profesa Lipumba kuwa mwenyekiti wa CUF.