Profesa Lipumba ataja vigogo waliotimuliwa CUF

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba amewataja viongozi wengine na wanachama wa chana hicho waliofukuzwa uanachama akiwamo aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amewataja viongozi na wanachama wengine waliofukuzwa uanachama katika mkutano mkuu uliofanyika kati ya Machi 13 hadi 15, 2019.

Licha ya jana Jumatatu Profesa Lipumba kulieleza Mwananchi kuwa Maalim Seif Sharif Hamad ni miongoni mwa waliofukuzwa kutokana na mwenendo wake wa kukidhoofisha chama hicho pia wamo wengine.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya CUF, Buguruni jijini Dar es Salaam leo Jumanne Machi 19, 2019, Profesa Lipumba amewataja wanachama wengine ni Ismail Jussa, Salim Biman, Issa Kheri, Mohammed Nur na Said Ali Mbarouk wote wa Zanzibar, Tanzania bara ni Mbarala Maharagande, Abdallah Katawi na Joran Bashange.

Hata hivyo, baadhi ya wanachama hao waliofukuzwa tayari leo Jumanne wamekabidhiwa kadi za chama cha ACT- Wazalendo akiwamo Maalim Seif.

"Mkutano mkuu umeazimia kuwafukuza uanachama kutokana na mwenendo wao usioridhisha na kuwa karibu na Maalim Seif ambaye amesababisha CUF kudhoofika," amesema Profesa  Lipumba.

Profesa Lipumba ambaye ni mtaalamu wa uchumi, amewataka wanachama wa CUF hasa Zanzibar kuacha kufuata mkumbo kwenda chama kingine badala yake wabakie CUF ili kuijenga

"Msimfuate Maalim Seif bakini tuijenge CUF, tumetoka mbali hasa wanachama wa Pemba. Maalim Seif ni mharibifu na ameangukia ACT- Wazalendo ambayo ipo mahututi," amesema Profesa Lipumba.