Profesa Mwandosya aja na mambo 10 kuinua uchumi

Tuesday June 2 2015

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu)

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) Profesa Mark Mwandosya akiwahutubia wanaCCM katika Uwanja wa Mkapa, Mbeya jana. Picha na Brandy Nelson 

By Lauden Mwambona na Brandy Nelson, Mwananchi

Mbeya. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu), Profesa Mark Mwandosya jana alitangaza nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  na kusema kesho atachukua fomu za kuwania nafasi hiyo.

Profesa Mwandosya alisema atachukua fomu katika Makao Makuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kesho saa nne asubuhi mjini Dodoma.

Akitangaza nia hiyo jijini Mbeya, Profesa Mwandosya alianza kwa vijembe, akisema alikuwa kimya kutangaza nia hiyo kama neema tu ya Mungu. Alisema katika maisha ni afadhali kuwa kimya kuliko kuwa mpayukaji na mwenye uamuzi wa papo kwa papo yenye hasara kwa Taifa.

“Mara nyingi katika maisha mjenga hoja na mtendaji makini ni bora kuliko mpayukaji mwenye maamuzi ya papo kwa papo na kusababisha hasara kwa Taifa,’’ alisema.

Alisema kipindi cha mpito katika Serikali nyingi ni kigumu, hivyo misingi ya waasisi wa Taifa inachangia Watanzania kuendelea kuwa na furaha.

CCM haiyumbi, bali wanachama

“Wapo wanaosema CCM inayumba, lakini mimi nasema CCM haiyumbi isipokuwa baadhi ya wanachama wake ndiyo wanaoyumba mno baada ya kukiuka kiapo cha ahadi za CCM ikiwamo inayokataza rushwa,’’ alisema na kuzisoma ahadi zote za CCM:

“Ahadi ya kwanza inasema; ‘binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja. Ahadi ya pili; ‘nitaitumikia nchi yangu na watu wake wote, ya tatu; ‘nitajitolea nafsi yangu kuondosha umaskini, ujinga, magonjwa na dhuluma’ ya nne; ‘rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa’.” Alisema na kueleza kwamba mbali ya ahadi hiyo, wengi wameikiuka na hivyo wanayumba.

Alitaja ahadi nyingine kuwa ni ya tano isemayo; ‘cheo ni dhamana, sitatumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu,’ ya sita; ‘nitajielimisha kwa kadri ya uwezo wangu na kuitumia elimu yangu kwa faida ya wote,’ ya saba inasema; ‘nitashirikiana na wenzangu wote kujenga nchi yetu, ya nane; ‘nitasema kweli daima, fitina kwangu mwiko na ya tisa inasema; ‘nitakuwa mwanachama mwaminifu wa CCM na raia mwema wa Tanzania na Afrika.’

Profesa Mwandosya aliwaambia mamia ya wanannchi waliokuwa wamefurika kwenye Uwanja wa Mkapa kwamba wana CCM wengi wamekiuka ahadi hizo ambazo waliapa mbele ya Watanzania na Mungu na kwamba ndiyo maana wanayumba wao, lakini CCM ipo imara.

Sababu za kugombea

Alisema ameamua kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho ili kuhakikisha Dira ya Maendeleo ya 2025 ambayo alishiriki kuiandaa mwaka 2000, inatekelezwa na kuifanya Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati na hatimaye mwaka 2050 iwe nchi ya dunia ya kwanza.

“Sasa tutafikaje huko, wengi wanaweza kuuliza,” alisema na kueleza kuwa ameandaa mambo 10 ya kutekeleza ili kufikia malengo hayo.

Profesa Mwandosya aliyataja mambo hayo kuwa ni pamoja na kuanzisha kilimo cha kisasa na kisayansi kinachozingatia sifa zote za kilimo cha kisasa kwa kuboresha pembejeo na miundombinu yote ya shughuli za kilimo.

Alitaja suala la pili kuwa ni kupambana na rushwa kwa kuondoa vikwazo vinavyozuia mapapa wa rushwa wasishughulikiwe na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Upo utaratibu kwamba kabla ya kuhojiwa, vigogo wala rushwa, lazima Takukuru wapate kibali, lakini kwa wala rushwa wadogowadogo  wao wanakamatwa na kufikishwa mahakamani bila kizuizi hicho, sasa hilo ni kero,’’ alisema.

Alisema akifanikiwa kupita na kuingia Ikulu, ataboresha sheria ili vigogo wa rushwa kubwa washughulikiwe kuliko wadogo ambao wataacha wenyewe.

Pia alisema akifanikiwa katika safari yake hiyo, atahakikisha vyombo vya kiuchumi kama Benki Kuu ya Tanzania (BoT), mifuko ya hifadhi inapewa uhuru zaidi wa kujisimamia na kwamba Serikali itakuwa mhimili wa uchumi ili kuwafanya Watanzania waone matunda ya kukua kwa uchumi.

“Serikali itakuwa injini ya kukua kwa uchumi kwa kuboresha mazingira ili sekta binafsi zifanye kazi kwa ufanisi na kulipa kodi nzuri kwa Serikali,’’ alisema.

Profesa Mwandosya alisema uchumi ukizorota Serikali, haiwezi kutekeleza majukumu na kwamba zilizotangulia zilifanya kazi nzuri kwa kujenga misingi ya uchumi.

Alisema mambo mengine ya kutekeleza ni kuanzisha na kuendeleza viwanda vya kuongeza thamani ya mazao ya kilimo na kuhimiza zaidi kilimo cha umwagiliaji ili nchi ijitosheleze kwa chakula na kuuza mazao yaliyosindikwa nje ya nchi.

Hatua nyingine ni kuondoa vizuizi vya uwekezaji kwa Watanzania na hata wa nje, kuimarisha sekta ya utalii wa ndani na nje kwa vile una fursa nyingi na pia kuhakikisha sekta ya utumishi inaboreshwa ili wafanyakazi waongeze bidii, uadilifu na kujituma kazini.

Profesa Mwandosya alisifia Serikali ya Rais Jakaya Kikwete kwamba imefanya mengi mazuri, lakini Watanzania wengi hawathamini wakati viongozi na watu mbalimbali wa nje ya nchi wanashangaa kwa ufanisi wa kazi hiyo.

Alisema Tanzania inaendelea vizuri katika kukua uchumi wake na kwamba yeye atasimamia kwa nguvu zote kuhakikisha uchumi unazidi kupanda chati hadi kuwafikia Watanzania wote.

“Baada ya uchumi kukua nitahakikisha elimu inaboreshwa kwa kuangalia sera na mitalaa na ikiwezekana elimu ya msingi itaanza darasa la kwanza hadi la kumi, lakini baadaye litakuwa hadi la 12,’’ alisema.

Alisema katika hili, pia atasimamia kuboreshwa kwa masilahi ya walimu na taaluma yao. Pia, baada ya uchumi kukua atahakikisha sekta ya afya inaboreshwa kwa kusimamia zaidi kitengo cha kinga akisema ni bora kuliko tiba.

“Kwa kweli siku hizi maofisa afya hawaonekani mitaa lakini utafika wakati tutalazimika kuimarisha zaidi kinga.’’

Profesa Mwandosya aligusia pia kwamba Serikali yake itaendelea kuimarisha ulinzi na usalama wa nchi na kuhakikisha Watanzania wanakuwa wamoja.

Alisema ulinzi wa Taifa na wananchi ni suala la lazima na kwamba akifanikiwa Serikali itaendelea kuliboresha.

Kuhusu ajira kwa vijana, alisema wasomi wanaotembea na vyeti mikononi kutafuta ajira wanapoteza muda na kuwataka vijana wa aina hiyo wawe wabunifu na wenye mawazo ya kujiajiri.

Aliwataka vijana wenye mawazo na fikra za kutaka kufanya kazi ya kujiajiri wafike kwake na watasaidiwa kupata fedha, lakini siyo kuomba kazi.

“Vijana jitumeni, hata kama mnakosa kazi Tanzania, wasomi nendeni Uarabuni, Zambia na Malawi kutafuta  kazi, jifunzeni lugha mbalimbali za kimataifa kikiwamo Kichina,’’ alisema na kuongeza kwamba wasomi wengi wa Kenya, Uganda , Ghana na Nigeria wamejaa nchi za mbali kufanya kazi.

Profesa Mwandosya alizungumzia pia suala la Muungano wa Tanganyika na Zanzibar akieleza kuwa ataudumisha kwa nguvu zote ili uwe wa kuigwa Afrika.

Alisema kwa kawaida visiwa vingi duniani ni chimbuko la maendeleo, hivyo anaamini Zanzibar inaweza kuwa kitovu cha maendeleo ya Tanzania.

“Zanzibar ikiwa na rasilimali watu, ikitumiwa vizuri itakuwa kitovu cha maendeleo ya nchi yetu,’’ alisema.

Sababu za kutangaza nia Mbeya

Kuhusu sababu za kutangaza nia ya kuchukua fomu za urais jijini hapa Profesa Mwandosya alisema alizaliwa Mbeya miaka 68 iliyopita na kusoma Shule ya Msingi Majengo. Aliishi eneo hilo kwa kipindi kirefu.

Profesa Mwandosya alisema mbali na yeye kuishi jijini Mbeya pia Baba wa Taifa Marehemu Julius Nyerere alikuwa akifanya mikutano yake eneo la viwanja hivyo wakati alipokuwa akidai uhuru wa Tanganyika.

“Eneo hili enzi hizo lilikuwa likiitwa Welfare Center, hivyo Waafrika walikuwa wakikusanyika hapa kumsikiliza Mwalimu Nyerere,’’ alisema.

Awali, watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya Mkoa wa Mbeya waliwasili na kuelezea matumaini yao kwa Profesa Mwandosya.

Wazanzibari watinga Mbeya

Katika hali isiyotarajiwa Wazanzibari zaidi ya 10 walitua jijini hapa wakiwa wamevalia fulana zilizoandikwa “Matumaini ya Zanzibar yapo kwa Profesa Mwandosya.’’

Wazanzibari hao wengi wao wakiwa wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, walisema walifika Mbeya kwa vile wanamwamini Profesa Mwandosya kwamba anaweza kuisaidia Tanzania Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Pia, alikuwapo Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa ambaye alisema kwamba Profesa Mwandosya anafaa kuongoza Tanzania kwa kuwa ana uelewa na mtazamo wa maendeleo ya kweli.

Ajibu maswali

Alipoulizwa atawafanyia nini Watanzania ili kuwaongezea imani alisema Profesa Mwandosya alisema: “Nitasimamia utawala bora na kuishi kwa kufuata haki na amani. Siamini katika utajiri wa kuwagawia wananchi.”

Kuhusu amelifanyia nini Taifa kwa kipindi chote alichokuwa mtumishi wa Serikali alisema: “Nimeyafanya mengi na wenzangu, sina nilichofanya peke yangu. Niliwahi kwenda kwenye shule moja ambayo niliichangia fedha nyingi na wakataka shule ile iitwe jina langu lakini nilikataa,” alisema na kuongeza: “Nilikataa kwa sababu hata kama kiongozi anabuni miradi mbalimbali, utekelezaji ni wa watu tofauti.”

Hata hivyo, aliwataka watu wanaotaka kujua zaidi mchango wake kwa jamii kwenda wizarani au kwenye taasisi mbalimbali alizowahi kufanyia kazi kuzitafuta na akawataka Watanzania wajenge desturi ya kujisomea vitabu ili kujua waliyofanya na watu tofauti.

Advertisement