Profesa Ndalichako ataka maonyesho vyuo vikuu kufanyika Dodoma

Saturday July 20 2019

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam.  Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia,  Profesa Joyce Ndalichako amefunga maonyesho ya 14 ya vyuo vikuu huku akiitaka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kufikiria namna ya kupeleka maonyesho yake ya  15 jijini Dodoma.

Pia, amevitaka vyuo kuendelea kutoa elimu inayochochea matumizi ya teknolojia ya kisasa katika kutatua matatizo ya jamii.

Ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Julai 20, 2019 katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam wakati akifunga maonyesho hayo yaliyoshirikisha  vyuo  81 kutoka ndani na nje ya nchi.

Amesema kutokana na Serikali kuhamia jijini Dodoma, sasa ni wakati wa kufikiri maonyesho hayo kufanyika Dodoma.

“Kama shughuli zetu ziko Dodoma hivi sasa hivyo ni vyema nanyi mkaanza kufikiri juu ya maonyesho ya 15 yatakavyofanyika Dodoma,” amesema.

Akizungumzia vyuo  kuhamasisha matumizi ya sayansi na teknolojia amesema kufanya hivyo i ni msaada kwa Taifa hasa kwa kuzingatia dira yake ya kuelekea uchumi wa viwanda katika mwaka 2025.

Advertisement

Awali, Katibu mkuu wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema vyuo 81 vimeshiriki  maonyesho ya mwaka 2019, kutoka ushiriki wa vyuo 73 mwaka 2018.

“Hii ni ishara kuwa maonyesho yanazidi kukua kila mwaka na tunategemea idadi hiyo kuongezeka zaidi mwakani,” amesema Profesa Kihampa.

 


Advertisement