Profesa Ndalichako azungumzia umuhimu wa maktaba mtandao

Waziri wa Elimu Profesa Joyce Ndalichako akijaribu kununua kitabu cha hadithi cha Kuku na Kanga kupitia maktaba mtandao ya Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) iliyozindulia leo jijini Dar es Salaam. Aliyeshika Kompyuta ni Mtaalamu wa IT wa taasisi hiyo, Calvin Msangi.

Muktasari:

Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako amesema kuanzishwa kwa maktaba mtandao kutawalazimisha walimu na wadau wengine wa elimu kuanza kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika ufundishaji


 Dar es Salaam. Waziri wa Elimu, Profesa Joyce Ndalichako amesema kuanzishwa kwa maktaba mtandao kutawalazimisha walimu na wadau wengine wa elimu kuanza kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) katika ufundishaji.

Amesema maktaba hiyo ni suluhisho katika kufikisha mapema vitabu shuleni kutokana na kuwepo kwa changamoto ya ucheleweshwaji katika baadhi ya maeneo.

Akifungua maktaba mtandao leo Jumamosi Machi 30, 2019 Profesa Ndalichako amesema kupitia maktaba hiyo walimu watalazimika kuanza kufundisha kwa kutumia teknolojia ya kisasa ya Tehama.

"Hii in fursa nyingine kwa walimu na niseme tu, shuleni za Serikali sio kwamba watapata bure kabisa hapana zitalipitiwa kupitia elimu bila malipo, Serikali itailipa taasisi," amesema Ndalichako.

Waziri huyo wa elimu amesema kuanzishwa kwa majtaba hiyo inayoendeshwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) hakutazuia usambazaji wa vitabu vya kawaida.

Alizitaka halmashauri za wilaya, miji na majiji zilizofungia vitabu makabatini kusambaza shuleni kwa madai kuwa hiyo pia ni sababu ya ucheleweshaji wa vifaa hivyo vya kufundishia.

Ndalichako ambaye wakati wa uzinduzi alinunua kitabu cha hadithi cha kuku na kanga kupitia mtandao aliwataka walimu kuchangamkia maktaba hiyo ili wamalize changamoto ya uhaba wa vitabu shuleni.

Awali,  Mkurugenzi Mtendaji wa TET, Aneth Komba amesema tayari walimu 88,566 wameshasajiliwa na wanaweza kuanza kununua vitabu hivyo.

"Taasisi imesogeza huduma ya vitabu karibu kwa hiyo ni rahisi kuvipata," amesema.

Kaimu Ofisa Elimu Msingi katika wilaya ya Kinondoni Chitegetse Dominick amesema maktaba mtandao itawarahisishia kazi walimu hasa katika kuandaa masomo yao.

"Kwa hiyo mwalimu akiwa na simu yake popote anaweza kununua na kukitumia kitabu, hii ni fursa adhimu," alisisitiza Dominick.

Kupitia maktaba hiyo shule binafsi wanaweza kununua vitabu kwa gharama isiyozidi 400,000 itakayowawezesha kupaya kopi za kiada 48 na ziada 2,000.