VIDEO: Profesa wa elimu aibua mjadala lugha ya kufundishia

Muktasari:

  • Kauli ya Profesa Omari kutaka mjadala wa elimu ambao pamoja na mambo mengine unapaswa kujadili hatima ya lugha ya kufundishia, imekuja huku marais wawili wastaafu kwa nyakati tofauti wakigusia haja ya kuwapo kwake.

Dar. Msomi maarufu nchini Profesa Issa Mcholo Omari (pichani) amekazia haja ya kuwapo kwa mjadala wa kitaifa kuhusu elimu, huku akionya kuwa Tanzania itafanya kosa ikiwa itaruhusu matumizi ya Kiswahili kama lugha ya kufundishia shuleni na vyuoni.

Akizungumza na Mwananchi katika mahojiano maalumu, msomi huyo aliyebobea katika fani za saikolojia ya elimu, utafiti, tathmini na upimaji wa elimu, alisema hajaona sababu za kielimu au ya kimaendeleo ambazo zinailazimisha Tanzania kutumia Kiswahili kufundishia.

“Hatuwezi kuwa na elimu bora kwa sababu ya kubadili lugha ya kufundishia kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili na tukibadili ni lazima kama nchi tujiandae kushuka kielimu kwa kiasi kikubwa,” alisema Omari aliyekuwa Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa takriban miaka 30.

Aliongeza, “Kiingereza ni lugha ya ulimwengu, hivyo kuacha kuitumia inamaanisha Watanzania hasa vijana watakosa nafasi ya kufanya kazi kwenye ulimwengu wa leo. Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa Kiingereza ni lugha ya ulimwengu siyo ya Uingereza.”

Kauli ya Profesa Omari kutaka mjadala wa elimu ambao pamoja na mambo mengine unapaswa kujadili hatima ya lugha ya kufundishia, imekuja huku marais wawili wastaafu kwa nyakati tofauti wakigusia haja ya kuwapo kwake.

Novemba 11, 2017, Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa alisema kuna haja ya kuutafakari upya mfumo wa elimu na kushauri kuanzishwa kwa mjadala utakaojumuisha makundi mbalimbali.

Alitoa kauli hiyo katika kongamano la wanataaluma lililofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).

Aprili 18, 2018, Rais aliyemfuatia Jakaya Kikwete akagusia suala hilo alipokuwa akizungumza katika kongamano lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Havard nchini Marekani.