RC Dodoma aitaka Vodacom kuboresha huduma

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ameitaka Kampuni ya Simu ya Vodacom Plc kuwekeza katika mawasiliano ili kuondokana tatizo la kukatikakatika kwa mtandao kwenye baadhi ya maeneo mkoani humo

Dodoma. Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Binilith Mahenge ameitaka Kampuni ya Simu ya Vodacom Plc kuwekeza katika mawasiliano ili kuondokana tatizo la kukatika katika kwa mtandao kwenye baadhi ya maeneo mkoani humo.

Dk Mahenge ameyasema hayo leo Alhamisi Mei 9, 2019 akizindua duka na ofisi za kampuni hiyo ambalo litatoa huduma mkoani Dodoma na Singida.

Dk Mahenge amesema katika baadhi ya maeneo mtandano wa simu umekuwa haufanyi kazi akidai kuwa mawasiliano yamekuwa yakikatika.

“Wekezeni katika mawasiliano wakati mwingine mtandao umekuwa unakatika, huduma sio nzuri katika baadhi ya maeneo,” amesema.

Mbunge wa Dodoma Mjini (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Anthony Mavunde amesema kampuni hiyo ni sehemu ya mafanikio ya mpango wake kugawa kompyuta kwa kila shule jimboni kwake kwa ajili ya kuwezesha wanafunzi kujifunza kwa teknolojia.

Akizungumza katika hafla hiyo, mkurugenzi wa uhusiano na mawasiliano wa Vodacom Tanzania Plc,  Rosalynn Mworia amesema huduma za mawasiliano ni muhimu katika kuchochea maendeleo na ukuaji uchumi.

 “Tumeona umuhimu wa kuongeza nguvu Dodoma kwa kufungua ofisi zetu na pia kuongeza duka jipya nia yetu ikiwa kuchochea shughuli za kiuchumi za mkoa huu,” amesema.

Amesema kampuni hiyo ina minara zaidi ya 50 inayotoa huduma ya mtandao wa 4G na bado wataongeza saiti nyingine 10 hivyo wakazi wa Dodoma watapata huduma zote za mawasiliano ya kidijitali kwa urahisi na ukaribu zaidi.