RC Hapi azindua jukwaa la Naweza Iringa

Friday March 15 2019

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi(wa pili

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi(wa pili kulia)  akisisitiza jambo kwa wadau wa Afya wa Mkoa wa Iringa (hawapo pichani) mara baada ya kuzindua Jukwaa la “NAWEZA” litakalozungumzi maswala ya Afya kwa watu wazima hususani Afya ya Mama na Mtoto.Kulia ni Mwakilishi kutoka USAID Tulonge Afya, Jacqueline Larsen,Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela na Mwakilishi kutoka USAID, Ananthy Thambiayagam.Uzinduzi huo umefanyika leo Mkoanim humo. 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amezindua Jukwaa liitwalo ‘Naweza’ litakaloshughulikia masuala ya afya kwa watu wazima hususan afya ya mama na mtoto mkoani humo.

Lengo la jukwaa hilo alilozindua jana, Alhamisi, Machi 14, 2019 ni kufikisha elimu sahihi itakayowajengea uwezo wananchi kubadili tabia na mtazamo hasi ili kuleta matokeo chanya ya kiafya.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Hapi alisema lengo la Serikali ni kupunguza vifo vya uzazi na watoto wachanga vinavyosababishwa na changamoto mbalimbali zikiwemo huduma duni  na ukosefu wa elimu, matumizi sahihi ya huduma za afya na afya ya uzazi.

Alisema serikali kwa kushirikiana na mradi wa USAID Tulonge Afya fhi 360 inajitahidi kuelimisha jamii juu ya afya ya uzazi katika kupunguza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, vifo vya watoto wachanga na vile vinavyotokana na ugonjwa wa malaria.

Katika uzinduzi huo, Hapi alisema vyombo vya habari vina jukumu la kuisaidia Serikali kufikisha ujumbe na elimu sahihi kwa wananchi na jamii, ili wapate uelewa na umuhimu wa kuwa na afya bora itakayowawezesha kushiriki shughuli za uzalishaji na kuinua uchumi.

Mkuu huyo wa mkoa alisema jukwaa hilo litatoa huduma jumuishi za afya katika maeneo ya afya ili kuiwezesha Serikali kufanikisha mikakati na vipaumbele vyake vya kupunguza maambukizi ya virusi vya Ukimwi, vifo vya akinamama vitokanavyo na uzazi, vya watoto wachanga, malaria na kifua kikuu (TB).

Alisema kukosekana kwa taarifa sahihi za masuala ya afya kumesababisha wananchi wengi wakose elimu sahihi ya afya ya uzazi na hivyo kushindwa kubadili tabia zao.

Advertisement