RC Kagera ataka kiama kwa viongozi wanaohujumu Kahawa

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Brigedia Jenerali Marco Gaguti ametangaza kiama kwa viongozi wanahujumu mfumo wa ununuzi wa kahawa na kusababisha malalamiko yasiyokoma katika ofisi yake

Karagwe. Malalamiko ya wananchi kuhusu mwenendo wa bei ya kahawa yamemtisha Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti na kutangaza kiama kwa viongozi aliodai wanahujumu shughuli hiyo zima na kusababisha wananchi kukosa imani na Serikali.

Akifungua Mkutano Mkuu wa Chama kikuu cha ushirika Karagwe(KDCU) leo Jumanne Machi 5,2019 amesema anapokea malalamiko mengi ya wakulima na kuwanyoshea kidole viongozi ndani ya Serikali na chama aliosema wanahujumu ununuzi wa kahawa na kuchelewesha malipo kwa maslahi yao binafsi.

Amesema msimu uliopita walipata taabu kutokana na hujuma mbalimbali huku akionya kuhusu harufu ya mgawanyiko inayonukia katika chama hicho kwa kuibuka ajenda za kujitenga ambapo KDCU inaundwa na wakulima wa Wilaya za Karagwe na Kyerwa.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kyerwa (CCM) Innocent Bilakwate amejilipua kwa viongozi wa vyama vya msingi vinavyounda ushirika huo akisema wengi wao ni wezi wanaonyonya wakulima na kuwa hajali kusema ukweli uliopo.

Pamoja na udhibiti mkali uliopo Mkuu wa Wilaya ya Karagwe, Godfrey Mheluka amesema kahawa inatoroshwa kwenda nchi jirani na wanaokamatwa wanadai wanakwenda kulipa madeni.

Amedai wiki hii limekamatwa gari aina ya Noah likitorosha kahawa kwenda nchi jirani ya Uganda na watuhumiwa kudai walishachukua fedha huku akidai udhibiti unaoendelea umesaidia chama hicho kuvuna faida ya zaidi ya Sh200 milioni kabla ya hapo misimu yote walipata hasara

Kupitia mfumo mpya wa ununuzi wa kahawa vyama vya ushirika vimebaki kuwa wakusanyaji na kupeleka zao hilo sokoni na sio kuwa wanunuzi kama awali ambapo msimu uliopita bei ya awali ilikuwa Sh1,000 kwa kahawa zote robusta na arabika.