RC Mbeya: Mikakati ya kumng’oa Sugu imeiva

Wafuasi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na watumishi wa serikali wa mkoa wa Mbeya wakiwa na mabango waliposhiriki kwenye maandamano ya kumpongeza Rais John Magufuli kwa utendaji kazi tangu aingie madarakani .Picha na Ipyana Samson

Muktasari:

  • Matembezi hayo yaliandaliwa na CCM Mbeya Mjini na uongozi jiji la Mbeya na watumishi wa jiji hilo walitangaziwa na mkurugenzi mtendaji wa jiji, James Kasusura kushiriki kumpongeza Magufuli.

Mbeya. Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema matumaini ya kulikomboa jimbo la Mbeya Mjini kutoka mikononi mwa upinzani kwenda CCM yameiva kutokana na mipango mikakati thabiti ya chama hicho ya kuhakikisha jimbo hilo linaongozwa na chama tawala.

Amesema wananchi wa jimbo hilo wameonyesha kuridhishwa na utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli na namna anavyoitendea haki Ilani ya CCM ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Chalamila alisema hayo jana wakati akituhubia watumishi wa Serikali, wanachama wa CCM na wakazi wa jiji la Mbeya katika makao makuu ya CCM yaliyopo Sabasaba jijini hapa baada ya kupokea maandamano ya amani yaliyoanzia viwanja vya Ruanda Nzovwe hadi Sabasaba kwa lengo la kumpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya kuwatumikia Watanzania.

Matembezi hayo yaliandaliwa na CCM Mbeya Mjini na uongozi jiji la Mbeya na watumishi wa jiji hilo walitangaziwa na mkurugenzi mtendaji wa jiji, James Kasusura kushiriki kumpongeza Magufuli.

“Mimi nitaondoka Mbeya baada ya kuhakikisha wananchi wote ni kijani tena nitaondoka madarakani nikiwa tayari nimefikisha miaka 60. Hivyo wakazi wa jiji la Mbeya tuendelee kuunga mkono juhudi za Rais wetu kwani amewaletea vitambulisho vya ujasiriamali na mimi nimewatengea maeneo ya kufanya biashara zenu kwa uhuru,” alisema.

“Rais ametoa fedha Sh300 bilioni kwa ajili ya maendeleo mbalimbali kwenye mkoa wetu ikiwamo ujenzi wa barabara, vituo vya afya, ujenzi wa shule na miradi maji,” aliongeza.

Naye katibu wa CCM mkoa wa Mbeya, Solomon Itunda alisema wamefikia uamuzi wa kufanya maandamano ya amani baada ya kuridhishwa na utendaji kazi uliotukuka wa Serikali ya awamu ya tano.

“Sisi wananchi wa Mbeya tumeandamana kumpongeza Rais kwa sababu amenunua ndege ambazo hata sisi tunanufaika nazo, kaleta fedha za ujenzi wa vituo vya afya kwenye kila kata na zahanati kila kijiji, elimu bure pamoja na ujenzi wa madarasa ya shule za msingi na sekondari,” alisema.

Naye Kasusura alisema jiji hilo tangu awamu ya tano iingie madarakani limejenga vituo vitatu vya afya, ujenzi wa barabara za mchepuko katikati ya jiji na ukarabati wa shule ya awali ya Azimio pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa shule za sekondari.

Maandamano hayo pia yaliwashirikisha wanafunzi wa shule za sekondari zinazomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi CCM, wanafunzi wa vyuo mbalimbali vikuu na vya kati vilivyopo mkoani hapa, wapiga debe wa vituo vya mabasi vya Uyole, Nanenane, Kabwe na Stendi Kuu. Jimbo la Mbeya mjini mbunge wake ni Joseph Mbilinyi au Sugu.