RC Mnyeti amtaka mkuu wa wilaya kujitathmini

Tuesday February 12 2019Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti 

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti  

By Joseph Lyimo, Mwananchi [email protected]

Babati. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amemtaka mkuu wa wilaya ya Hanang' Joseph Mkirikiti kujipima kwa maelezo kuwa ameshindwa kugawa vyema vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo wa eneo hilo.

Wilaya ya Hanang' imekuwa ya mwisho katika ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo kati ya wilaya tano za mkoani Manyara. Kila wilaya ilipewa vitambulisho 5,000.

Akizungumza leo wilayani Babati, Mnyeti amempa wiki mbili Mkirikiti kusimamia vyema ugawaji wa vitambulisho 5,000 vya awali na vingine 6,619 alivyokabidhiwa hivi karibuni.

Amesema amesikitishwa na kauli ya wilaya hiyo kuwa haina wafanyabiashara wadogo wengi, wakati awali walitoa taarifa ya maeneo yao kuwa na wafanyabiashara wa kutosha na wakatoa na idadi.

"Mkuu wa wilaya ya Hanang' nakupa wiki mbili za kugawa vitambulisho hivyo na endapo utashindwa uandike barua ya kujipima kwa nini umeshindwa kutekeleza zoezi hilo la kitaifa," amesema Mnyeti.

Amewataka maofisa tarafa, watendaji wa kata, vijiji na watumishi wengine wa Serikali kutimiza wajibu wao ipasavyo katika kufanikisha zoezi hilo.

Advertisement

"Huko Hanang' ninyi ndiyo mliofanya tathmini si sisi wa mkoani mkatuletea idadi, inakuwaje mnashindwa kuwafikia wote. Fanyeni kazi kwa uhakika kwa kuwapatia wahusika vitambulisho vyao," amesema Mnyeti.

Kwa upande wake Mkirikiti amekiri ugawaji vitambulisho kusuasua ila wamepanga mikakati kuhakikisha wanafanya uhakiki na kuwapatia wafanyabiashara wadogo wanaostahili kupata vitambulisho hivyo.

Amesema awali walipokea vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo 5,000 lakini wakafanikiwa kuwapatia wafanyabiashara 2,247 kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo.

Wilaya ya Hanang' ina wafanyabiashara wadogo wengi kwenye miji midogo inayokuwa kwa kasi ya Katesh, Endasak, Bassotu, Nangwa, Simbay, Gidahababieg na Balang'dalalu.

 


Advertisement