RC aamuru watumishi wa umma kusalimisha ATM

Saturday May 25 2019

 

By Suzy Butondo, Mwananchi [email protected]

Kishapu. Serikali mkoani Shinyanya imeamua kuingilia kati kulinda masilahi ya watumishi wake ambao wamelazimika kusalimisha kadi zao za benki (ATM) kwa watu binafsi waliowakopesha akiwataka kuzikabidhi kwa wakuu wao.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Tellack alisema jana kuwa ofisi yake imeagiza kufanyika kwa uhakiki wa mikopo binafsi ya watumishi wa umma, hasa wale wa halmashauri waliobainika kukopa hadi kufikia hatua ya kukosa mishahara mwisho wa mwezi ili kulinda masilahi ya pande zote mbili; wakopaji na wakopeshaji.

“Wote wanapaswa kuzingatia sheria, si nia ya Serikali kuwafanya waliowakopesha watumishi kupata hasara. La Hasha! Tunataka kulinda haki na masilahi ya pande zote kwa mujibu wa sheria, ndiyo maana mwezi huu tumeruhusu hata watumishi ambao hawajaitikia agizo la uhakiki wa ATM Cards zao, walipwe mishahara yao.

Wilaya ya Kishapu mkoani humo imeshachukua hatua na hivi karibuni ilitoa tangazo ikiwataka watumishi wake kusalimisha kadi hizo za benki. “Utafiti uliofanywa na ofisi ya mkuu wa mkoa umebaini kuwa wapo watumishi 269 waliosalimisha kadi zao za benki kwa waliowakopesha na wahusika (wakopeshaji) wameagizwa kurejesha kadi hizo kwa wamiliki,” alisema Kaimu Mkurugenzi Mtendaji (DED) wa Wilaya ya Kishapu, Mang’era Mang’era juzi.

Alisema siku ya mwisho ya kutekeleza amri hiyo ilikuwa juzi Mei 23, 2019.

“Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kishapu anawatangazia kuwa watumishi wote mnatakiwa kuwasilisha kadi zenu za benki (ATM cards) makao makuu ya Halmashauri ya Kishapu siku ya Alhamisi tarehe 23/05/2019 kuanzia saa 2:00 asubuhi; NB: Kutokufika kwenye zoezi hilo mishahara yako itazuiwa,” linasomeka tangazo hilo lililosainiwa na Mang’era.

Advertisement

Akizungumza na Mwananchi kuhusu tangazo hilo, Mang’era ambaye pia ni ofisa mipango wa Kishapu, alisema uamuzi wa kuhakiki kadi hizo ni kutaka kudhibiti tabia ya baadhi yao kuchukua mikopo kutoka taasisi za fedha bila kuzingitia kanuni na taratibu.

“Wapo baadhi ya watumishi wamekopa hadi kufikia hatua ya kusalimisha kadi zao za benki kwa waliowakopesha, hasa kwenye kampuni na watu binafsi. Kiutaratibu, mtumishi akikopa benki au taasisi yoyote ya fedha, anatakiwa kubakiza angalau moja ya tatu ya mshahara wake baada ya marejesho kwa ajili ya mahitaji yake binafsi na familia. Lakini baadhi hawazingatii sharti hili,” alisema.

Alisema kitendo hicho kimefanya utendaji na ufanisi kazini kwa watumishi wenye mikopo ya aina hiyo kushuka kwa sababu badala ya kuelekeza akili na juhudi kazini, hutumia muda mwingi kufikiria watakavyomudu maisha.

Pamoja na kuchukua mikopo sehemu mbalimbali bila kuzingatia kanuni za utumishi, Mang’era alisema baadhi ya mikopo hiyo pia hutozwa riba kubwa kati ya asilimia 40 hadi 50.

Advertisement