RPC Mwanza aagiza mwandishi wa Mwananchi aachiwe

Muktasari:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,  Jumanne Muliro ameagiza mwandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) mkoani humo, Jonathan Mussa kuachiwa kwa dhamana

 


Mwanza. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,  Jumanne Muliro ameagiza mwandishi wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) mkoani humo, Jonathan Mussa kuachiwa kwa dhamana.

Musa anashikiliwa tangu jana Jumatano Februari 20, 2019  kwa mahojiano kuhusu taarifa za watu kudaiwa kukamatwa wakiwa na vichwa vya binadamu.

Taarifa hizo zilizozagaa na kuzua taharuki zilisababisha umati wa watu kujaa eneo la Kituo cha Polisi Nyakato jijini Mwanza kutaka kushuhudia vichwa hivyo na watuhumiwa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Februari 21, 2019, Muliro amesema Musa na mwandishi mwingine wa Star Tv, Sylveter Bulengela waneshikiliwa baada ya kudaiwa kuwa chanzo cha taarifa hizo kuenea mtaani.

"Kutokana na uhalisia wa tukio na taharuki iliyokuwepo niliagiza wote wanaowezekana kuwa chanzo cha taarifa hizo kukamatwa na kuhojiwa kupata ukweli," amesema Kamanda Muliro.

"Lakini suala lenyewe linadhaminika  na nimemwagiza RCO (Mkuu wa upelelezi Mkoa) ashughulikie waachiwe kwa dhamana.”

Wakati kamanda Muliro akisema waandishi hao walishikiliwa kwa tuhuma za kuwa chanzo cha taarifa zilizoibua taharuki, Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa (RCO), Faustine Mafwere amesema Musa anashikiliwa kwa kosa la kumpiga picha alipokuwa akizungumza na wananchi nje ya kituo hicho.

Katika maelezo yake hayo, RCO aliahidi kumwachia huru mwandishi huyo baada ya kuandika maelezo.