Radi yaua watano wa familia moja

Muktasari:

  • Watu watano wa familia moja wamefariki dunia na watatu kujeruhiwa kwa kupigwa radi wilayani Sikonge mkoa wa Tabora

Tabora. Watu watano wa familia moja wamefariki dunia kwa kupigwa na radi wilayani Sikonge mkoani Tabora.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Emmanuel Nley amesema leo Aprili 24  kuwa tukio hilo limetokea juzi saa 4:00 usiku katika kijiji cha Isongwa, kata ya Mkolye wakati mvua iliyoambatana na radi ikinyesha.

Amesema familia hiyo ilikuwa imelala na radi ilipiga kupitia dirishani na kupasua ukuta wa nyumba waliyokuwa wamelala.

Amewataja waliofariki kuwa ni mama mwenye nyumba, Muhindi Petro aliyeungua kifuani na paja la kulia, Vaileth Juma aliyeungua usoni, ziwa la kushoto na mkono wa kulia na Grace Juma aliyeungua usoni.

 

Wengine ni Kurwa Lukanya aliyeungua kifuani na mkono wa kushoto na Nyanzobe Juma aliyeungua usoni na mguu wa kulia.

Waliojeruhiwa ni Dotto Lukanya, Pendo Machia na Masanja Juma aliosema walipata majeraha madogo na walipata matibabu hospitali na kuruhusiwa.

Kamanda Nley amesema miili ya marehemu wote ilifanyiwa uchunguzi na wanandugu kuruhusiwa kuichukua kwa ajili ya maziko.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Peter Nzalalila amesema Muhindi alikuwa amelala na watoto wake katika chumba kidogo kwenye nyumba hiyo ya vyumba viwili.

Amesema mume wa Muhidi ana wake wawili na kwamba siku hiyo alikuwa kwenye nyumba nyingine nje ya wilaya ya Uyui na pia alikuwa ana mipango ya kuhamia.

Nzalalila amesema tukio hilo limewasononesha na kuwaachia majonzi makubwa wakazi wa kijiji hicho na halmashauri nzima ya wilaya ya Sikonge.