Rais Kabila aikamata tena Congo, alishika Bunge

Monday January 14 2019

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Mgombea urais wa muungano wa vyama vya upinzani, Martin Fayulu anataka atangazwe kuwa mshindi, akimtuhumu Rais Joseph Kabila kucheza rafu iliyomfanya Felix Tshisekedi, ambaye anaelewana naye, awe mshindi na hivyo kumrithi cheo chake.

Yaani anahisi Kabila anataka mtu aliyeingia naye makubaliano ndio awe mrithi wake baada ya kuiongoza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa miaka 18.

Hata hivyo, hata kama Fayulu atafanikiwa kugeuza matokeo hayo mahakamani, bado atakuwa na mtihani mwingine mkubwa wa kuiongoza nchi; kwa kuwa wagombea wa vyama vinavyomuunga mkono Kabila wameshinda zaidi ya nusu ya viti vyote vya ubunge na hivyo kumfanya rais huyo anayeondoka madarakani, akikamate chombo hicho cha kutunga sheria.

Wakati Fayulu anataka mahakama iamuru kura za urais zihesabiwe upya, wagombea 288 wanaomuunga mkono Rais Kabisa wameshinda viti vya ubunge kati ya 429 vilivyotangazwa hadi Jumamosi, huku wapinzani wakishinda viti 141 kati ya hivyo, kwa mujibu wa matokeo yaliyopatikana Tume Huru ya Uchaguzi ya Congo (Ceni).

Waziri wa Mawasiliano wa Congo, Lambert Mende alisema wanaomuunga mkono Rais Kabila walishinda viti 350 na wapinzani kupata 130.

Zaidi ya wagombea 15,000 wa ubunge walishiriki kwenye uchaguzi huo.

Ili kulikamata Bunge, chama kinatakiwa kipate zaidi ya viti 250 kati ya 500 vinavyotakiwa, na Kabila sasa atapumzika kwa starehe baada ya wafuasi wake kupata viti hivyo.

Kama matokeo hayo yakithibitishwa, wabunge wanaomuunga mkono Kabila watalikamata Bunge kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Nchi hiyo kubwa iliyo Kanda ya Kati ya Afrika, ikiwa na eneo linalolingana na Ulaya Magharibi, imekuwa katika mzozo kwa takriban miaka miwili kutokana na Kabila kukataa kuachia madaraka baada ya muda wake wa kikatiba wa vipindi viwili kumalizika mwaka 2016.

Uchaguzi wa Rais wa kumpata mrithi wake ulicheleweshwa mara tatu kabla ya kufanyika Desemba 30, siku ambayo pia ulifanyika uchaguzi wa wabunge.

Matokeo ya awali yaliyotangazwa Alhamisi iliyopita yalimpa Felix Tshisekedi, mtoto wa mwanasiasa maarufu wa upinzani wa zamani, Etienne Tshisekedi, ushindi wa asilimia 38.57 ya kura zote, akiwa amemzidi kidogo Fayulu, aliyepata asilimia 34.8. Mgombea urais kutoka chama cha Rais Kabila, Emmanuel Ramazani Shadary, alipata asilimia 23.8.

Matokeo hayo yalishangaza waangalizi wengi wa uchaguzi wa nchi hiyo yenye utajiri wa madini lakini ambayo umaskini umetamalaki na ambayo imekuwa katika vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka 22 pamoja na uchaguzi uliokuwa na umwagaji damu wa mwaka 2006 na 2011 ambao Kabila alishinda.

Ubashiri uliokuwepo kabla ya uchaguzi ulimpa Fayulu ushindi mkubwa huku wakosoaji wa Kabila wakihisi kuwa angechakachua matokeo ili kumpa ushindi Shadary.

Lakini wachambuzi wa mambo wanasema Kabila, 47, aliamua kutafuta njia ya kukwepa kusakamwa na jumuiya ya kimataifa, jambo ambalo lingefuata iwapo angechakachua matokeo na kumpa ushindi Shadary, ambaye alionyesha hadharani kuwa anamuunga mkono.

Kwa mujibu wa wachambuzi hao, baadaye aliingia katika makubaliano na Tshisekedi, ambaye ni kiongozi wa UPDC, chama kikongwe cha upinzani na kikubwa kuliko vyote.

Baadhi ya wachambuzi wanasema, Kabila aliomba kinga ya kutoshtakiwa kutokana na makosa aliyofanya katika miaka 18 ya utawala wake uliokuwa wa kimabavu na pia kuomba mali zake zisitaifishwe ili ampe ushindi Tshisekedi.

Kanisa Katoliki, ambalo lina nguvu kubwa nchini Congo, lilisema matokeo ya awali yaliyotangazwa na Ceni hayawiani na takwimu ambazo waangalizi wake 40,000 walikusanya kutoka vituoni.

Vyama vinavyomuunga mkono Fayulu, kikiwamo UNC vilisema Ijumaa kuwa kiongozi huyo ndiye mshindi wa kweli baada ya kupata asilimia 61 ya kura zote.

Sheria inawataka wagombea kuwasilisha rufaa ya kupinga matokeo ndani ya saa 48 na Mahakama ya Katiba inatakiwa itoe uamuzi ndani ya wikii moja.

“Hatutegemei uchaguzi ufutwe, bali kura zihesabiwe upya,” alisema Fayulu.

Siku ya kupiga kura ilikuwa na amani, lakini kukawa na wasiwasi kuhusu kuhesabu kura.

Hali hiyo imefinyisha matumaini ya nchi hiyo kushuhudia kwa mara ya kwanza mabadiliko ya uongozi ya amani tangu ipate uhuru mwaka 1960.

Rais Kabisa pia atakuwa amefarijika na kauli za China na Russia, ambazo zimeutaka Umoja wa Mataifa (UN) kukaa mbali na yanayoendelea nchini Congo.

Viongozi wengi wametaka mgogoro huo wa uchaguzi umalizwe kwa amani, lakini salamu hizo hazijawa na pongezi kwa Tshisekedi.

Kiongozi wa Ceni, Corneille Nangaa, akizungumza katika mkutano uliofanyika kwa njia ya video, aliomba jumuiya ya kimataifa kuunga mkono utawala mpya.

Askofu Marcel Utembi, kiongozi wa baraza la maaskofu wa Kanisa Katoliki, aliliomba Baraza la Usalama la UN kuitaka Ceni kutoa matokeo yanayolingana na yale yaliyohesabiwa vituoni.

Katika hatua nyingine, Russia na China zimesema katika mkutano wa Baraza la Usalama la UN kuwa mataifa yenye nguvu duniani yasijihusishe na mzozo uliopo Congo.

Waangalizi kutoka nchi za Magharibi wamehoji matokeo ya urais yaliyotangazwa Desemba 30, huku Ubelgiji na Ufaransa zikisema zinasubiri taarifa za kina kutoka vyombo vya uchaguzi kuhusu kura zilivyohesabiwa.

China na Russia ziliweka bayana kwamba UN inatakiwa ijihusishe zaidi na usalama wa Congo wakati ikijiandaa kushuhudia mabadiliko ya kwanza ya amani ya uongozi.

Balozi wa Russia, Vassily Nebenzia alisema “ubashiri” wowote kuhusu kura “haukubaliki” na unaweza kusababisha madhara makubwa nchini Congo na katika ukanda wa wa maziwa makuu.

Balozi wa China, Ma Zhaoxu alitaka Ceni ipewe heshima kamili.

“Tunaamini kuwa watu wa DRC wana uwezo na busara za kutatua matatizo yao kwa njia zao,” alisema.

Afrika Kusini, ambayo si mwanachama wa baraza hilo, ilishauri mataifa makubwa kuisaidia Congo, huku balozi Jerry Matjila akisisitiza kuwa Congo “imepoteza muda mwingi katika kusaka amani na usalama.

Jijini Kinshasa, Fayulu ameiomba Mahakama ya Kikatiba kufuta matokeo ya awali yaliyompa ushindi Tshisekedi, mwanasheria wake alisema juzi.

Ombi lake lilifunguliwa Ijumaa kabla ya muda wa saa 48 wa kuwasilisha rufaa ya kupinga matokeo ya uchaguzi kuisha.

“Maombi yetu ni kutaka kufutwa kwa matokeo yaliyompa ushindi Felix Tshisekedi,” alisema mwanasheria huyo, Toussaint Ekombe nje ya mahakama.AFP.

Advertisement