Rais Kenyatta amkana Jaguar, amwandikia barua Magufuli

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dany Kazungu, ofisini kwa Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es salaam, Julai 2, 2019. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Muktasari:

  • Kauli aliyoitoa Mbunge wa Starehe nchini Kenya , Charles Kanyi maarufu Jaguar ya kuwataka raia wanaofanya biashara kuondoka nchini humo ndani ya saa 24 wakiwamo Watanzania, imemfanya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kumwandikia barua Rais wa Tanzania, John Magufuli kumweleza maneno ya Jaguar yalikuwa ni yake binafsi.

Dar es Salaam. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemtumia ujumbe maalumu Rais wa Tanzania, John Magufuli unaoelezea msimamo wa Serikali yake kuhusu kukerwa na matamshi yaliyotolewa na Mbunge wa Starehe, Charles   Kanyi maarufu Jaguar.

Ujumbe huo wa maandishi umewasilishwa leo Jumanne, Julai 02, 2019 na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Dany Kazungu na kupokelewa Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Magufuli, ofisini kwa waziri mkuu Magogoni jijini Dar Es Salaam.

Wiki iliyopita, Jaguar alitoa matamshi akiwataka raia wa kigeni kutoka mataifa mbalimbali wanaofanya shughuli za kibiashara nchini Kenya wakiwemo Watanzania waondoke ndani ya muda wa saa 24 kauli iliyozua mjadala mkubwa.

Akipokea taarifa hiyo Majaliwa  amesema Watanzania wamefurahishwa na hatua mbalimbali zilizochukulia na Serikali ya Kenya dhidi ya mbunge huyo zinazodhihirisha matamshi hayo hayakuwa msimamo wa Serikali ya Kenya wala wananchi wake bali ulikuwa ni msimamo  binafsi wa mbunge huyo.

Amesema siku zote Watanzania na Wakenya wamekuwa huru kuishi na kufanya kazi au biashara katika nchi za Afrika ya Mashariki na pale yalipotokea matatizo au kutokukubaliana Serikali husika zilikaa mezani na kumaliza tofauti hizo.

"Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania ni wa karibu mno na wa kidugu kwani kuna baadhi ya makabila yapo katika nchi mbili hizi kama vile Wamasai na Wakurya na  Wajaluo  hivyo ushirikiano katika masuala ya mbalimbali yakiwemo ya  kibiashara na ya kijamii haukwepeki," amesema

Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi na wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) kujiepusha na kauli zenye viashiria vya kujenga chuki, uhasama na migongano miongoni mwa wananchi kwani  kauli hizo zisipodhibitiwa mapema zinaweza kusababisha hofu na kutokuelewana miongoni mwao.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi Watanzania kuendelea kuishi kwa amani na upendo na ndugu zao wa Kenya na wageni wote kutoka nchi za EAC na duniani kwa ujumla ambao wapo nchini wakifanya shughuli mbalimbali kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Mambo yetu yote katika nchi za Afrika ya Mashariki  hasa ya biashara na ya  kiuchumi kwa ujumla yataenda vizuri endapo  tutalinda na kudumisha amani, bila amani tutaogopana na tutashindwa kabisa  kushirikiana,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu  ameahidi Serikali ya Tanzania kamwe haitaruhusu wala kufumbia macho kauli au vitendo vyovyote vyenye viashiria vya uchochezi dhidi ya nchi jirani  ili na kulinda na kuunga mkono juhudi mbalimbali za ushirikiano wa kisiasa na kiuchumi zinazofanywa na viongozi  wakuu wa Mataifa ya Afrika.

Kwa upande wake, Balozi Kazungu amemshukuru Waziri Mkuu Majaliwa kwa kauli yake aliyoitoa Bungeni jijini Dodoma iliyowataka Watanzania kuwa watulivu na wayachukulie matamshi ya Mbunge wa jimbo la Starehe nchini Kenya, Njagua kuwa ni msimamo wake binafsi na siyo  msimamo wa Wakenya na Serikali yao.

Balozi Njagua amesema msimamo wa Rais Kenyatta siku zote umekuwa ni kuwapokea na kuwakubali ndugu zao  wote wanaotoka nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki walioamua kuishi au kufanya biashara nchini Kenya.