Rais Magufuli aambiwa anatisha, sio rahisi mtu kuropoka mbele yake

Muktasari:

 

  • Leo Jumatano Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais wa Tanzania, John Magufuli amekutana na viongozi madhehebu ya dini na wanazungumza masuala mbalimbali.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Wanawake wa Wakiislam Mkoa wa Dar es Salaam, Pili Abdallah amewaomba mawaziri kuwa na mazoea ya kukutana na viongozi wa dini ili kuwa na uhuru wa kuwaeleza masuala mengi ya kitaifa.

Wito huo ameutoa leo Jumatano Januari 23, 2019 kwenye mkutano  maalumu na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini kati yao na Rais Magufuli, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Pili amesema kuna masuala ambayo hayafai kuzungumza moja kwa moja na Rais, hivyo itakuwa rahisi kuyazungumza wakikutana na mawaziri.

”Rais naomba mawaziri nao waonane na viongozi wa dini kwa wakati wao kama ulivyokutana hivi, mawaziri wakiita vikao kama hivi tutaweza kusema mengi kwa sababu baba (Rais Magufuli) unatisha, siyo rahisi mtu kuropokaropoka, tunaweza tukawa na mengi lakini tukayafichaficha,” amesema mama huyo na kuongeza:

“Hata mimi nina mengi lakini kama ningempata waziri husika, tuko naye tungeweza kuongea mengi na ungefikishiwa mengi ya kutupeleka mbele.”  

Viongozi ambao wamehudhuria kwenye mkutano huo maalumu kwa makundi ni viongozi kutoka  Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), viongozi kutoka Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata), Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), viongozi wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT) na viongozi wa makanisa mengine.

Pia, wapo viongozi wa Serikali akiwamo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, katibu mkuu kiongozi, John Kijazi na mawaziri wa wizara mbalimbali.