Rais Magufuli alipatia gereza la Butimba magari, trekta

Muktasari:

Rais wa Tanzania, John Magufuli ametoa magari mawili na trekta moja kwa Gereza Kuu la Butimba jijini Mwanza


Mwanza. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametoa magari mawili na trekta moja kwa Gereza Kuu la Butimba jijini Mwanza.

Amesema magari na trekta hilo ni kwa ajili ya shughuli za uongozi  na uchumi kwa wafungwa na askari wa gereza hilo.

Akizungumza mara baada ya kusikiliza kero, changamoto na maombi kutoka kwa mahabusu, wafungwa na askari magereza, Rais Magufuli amesema Serikali inawathamini na kutambua kazi inayofanywa na askari magereza na kuwataka wasijisikie wanyonge.

“Askari Magereza nimewasikia kilio chenu. Ninyi hamna tofauti na majeshi mengine na hamwezi kufanya kazi kwa kulalamika kwa mateso wakati mimi nipo; nimeyasikia kero zenu naenda kuyashughulikia,” amesema Rais Magufuli leo Jumanne Julai 16, 2019.

Wakati akiahidi kushughulikia kero zao, mkuu huyo wa nchi amewaagiza askari magereza kutimiza wajibu wao ikiwemo kuhakikisha vitu visivyoruhusiwa haviingizwi gerezani.

“Kazi yenu ya kufanya kazi katika magereza ni ya wito, nimesikiliza kero zenu na naenda kuyafanyia kazi,” amesisitiza Rais Magufuli

Awali, mmoja wa askari, Sajenti Jonas Mabula alimweleza Rais Magufuli kuwa gereza hilo linakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa vyombo vya usafiri kwa ajili ya maofisa, mahabusu na wafungwa.

“Hata Mkuu wa gereza hana usafiri na hulazimika kuomba au kudandia lifti anapokwenda kwenye vikao vya kamati ya ulinzi na usalama,” amesema askari huyo huku akipigiwa makofi na na wafungwa, mahabusu na maofisa wenzake

Sajenti Mabula ambaye kwa mujibu wa maelezo yake ni mhitimu wa shahada (hakutaja fani yake) amemweleza Rais Magufuli kuwa wakati mwingine askari hujisikia unyonge mbele ya askari wa majeshi mengine ya ulinzi na usalama kutokana na hali ngumu wanayofanyia kazi.

“Hata hizi sare wakati mwingine tunajinunulia kwa sababu tunaipenda kazi yetu,” amesema Sajenti Mabula

Ametumia fursa hiyo kumwomba Rais Magufuli kusaidia kupatikana kwa gari la wagonjwa, gari la utawala, ujenzi wa nyuma za askari pamoja na upatikanaji wa vibali vya mradi wa kokoto ili kuwezesha ujenzi wa nyumba bora za askari na maofisa wa jeshi hilo.