Rais Magufuli asema watuhumiwa 300 wameachiwa huru

Thursday July 18 2019

Rais wa Tanzania, John Magufuli,ziara,Kongwa jijini Dodoma,gereza la Kasungamile na Geita

Rais wa Tanzania, John Magufuli  

By Baraka Samson, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema watuhumiwa 300 wameachiwa huru katika magereza mbalimbali nchini.

“Wilayani Bariadi wameachiwa 100, Mugumu huko Serengeti wameachiwa 52, Tarime sita, Bunda watuhumiwa 24 na Kahama watuhumiwa 43,” amesema Rais Magufuli leo Alhamisi Julai 18, 2019 wakati akizungumza na wananchi wilayani Kongwa mkoani Dodoma.

Mbali na kutaja idadi hiyo, kiongozi mkuu huyo wa nchi ameagiza Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na vyombo vingine vya ulinzi kupita magerezani kuzungumza na watuhumiwa ili kubaini wanaoshikiliwa kimakosa waachiwe huru.

Amesema baada ya kutoa maagizo kwa wizara hiyo alipokuwa mkoani Mwanza, maofisa wake walikwenda Gereza Kuu la Butimba jana Jumatano Julai 17, 2019  kukaa na watuhumiwa kwa saa saba, baada ya mazungumzo hayo waliachiwa.

Amesema baada ya maofisa wa wizara hiyo kutembelea  magereza mbalimbali, watuhumiwa 300 waliokuwa wanashikiliwa kimakosa wameachiwa huru, katika Gereza la Butimba wameachiwa 75.

Magufuli amesema  maofisa hao wanaendelea kupitia kila Gereza kufanya uhakiki wa wanaoshikiliwa kimakosa na leo watakuwa Gereza la  Kasungamile na Geita.

Advertisement

“Siwezi kutawala nchi yenye machozi na watu wanaosikitika kwa unyonge na unyonge wao ni wa kuonewa,” amesema Rais Magufuli.


Advertisement