Rais Magufuli awapongeza Mwinyi na Kikwete

Sunday May 19 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewapongeza Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete na Rais wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi kutokana na kushiriki kwao kikamilifu katika kukuza dini ya Kiislamu nchini.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo Jumapili Mei 19, 2019 katika mashindano ya 20 ya kusoma na kuhifadhi Quuran Afrika yaliyofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, yakiandaliwa na Taasisi ya Al-Hikma.

“Inawezekana ndiyo maana Mzee Mwinyi  amefikisha miaka 95 ni kutokana na imani yake na kumcha Mungu, hongera mzee Mwinyi, hongera sana Mzee Kikwete, hongera sana wazee wengine nimeamini kumcha Mungu kuna baraka zake,” amesema Magufuli.

Amesema kila mtu anapaswa kuishi kwa kadiri ya mapenzi ya Mungu huku akiwataka viongozi wa dini kuendelea kutoa mafundisho na kuwasisitiza waumini wao kuyaishi.

“Naipongeza taasisi ya Al-Hikma kwa kuandaa mashindano haya na ninawapongeza washiriki kwa sababu yanadhihirisha kutunza amani ya nchi yetu kwa sababu vitabu vyote vitakatifu vinafundisha juu ya amani ya umoja na Taifa.”

Amesema; “Palipo na amani ndiyo maana leo tumeweza kukaa hapo, ndiyo maana hatuulizani, wapo Waislam wengi lakini pia wapo waumini wa madhehebu mengine,” amesema Magufuli.

Advertisement

Advertisement