Rais Museveni kumtembelea Magufuli Chato

Muktasari:

 Unaweza kusema baada ya Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta kufanya ziara binafsi ya siku mbili nchini Tanzania sasa ni zamu ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni atakayefanya ziara binafsi ya siku moja nchini. Museveni anatarajiwa kuwasili Tanzania kesho Jumamosi Julai 13, 2019 na kuonana na rais John Magufuli aliyepo wilayani Chato Mkoa wa Geita.

Dar es Salaam. Rais wa Uganda,  Yoweri Museveni kesho Jumamosi Julai 13, 2019 atawasili nchini Tanzania kwa ziara binafsi ya siku moja.

Taarifa iliyotolewa leo Ijumaa Julai 12, 2019 na mkurugenzi  wa mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa Museveni atamtembelea Rais wa Tanzania, John Magufuli nyumbani kwake wilayani Chato Mkoa wa Geita.

Akiwa Chato, Museveni atafanya mazungumzo na mwenyeji wake huyo ambaye siku saba zilizopita alitembelewa na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta aliyekuwa na ziara ya siku mbili.